Na: Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro amehitimisha mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la KIWOHEDE Mama Justa Mwaituka ambae kwa pamoja wamekubaliana kuanza ujenzi wa jengo la kisasa la MKONO SHUFAA lenye thamani ya Sh.117 Milioni.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Muro alisema jengo hilo litajengwa wakati wowote kuanzia sasa katika Hospitali ya Wilaya ya Ikung kwa ajili ya kuratibu na kusimamia shughuli za upingaji wa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike na kiume na wanawake katika Wilaya ya Ikungi ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wilaya zinakomesha matukio na vitendo vya ukatili wa kijinsi kwa watoto na wanawake.
DC Muro alisema wao kama wiliaya wameona waweke utaratibu utakaotuwezesha kupambana na matukio yanayozidi kuongezeka ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto wetu na wanawake kwa kujenga mifumo imara ya kuratibu na kushughulikia changamoto hii ambayo imeendelea kuongezeka katika wilaya.
Muro aliongeza kuwa maono ya wilaya ni kuona wanabadili mwelekeo ambao hautamtazama mtoto wa kike peke yake bali utawatazama watoto wote kama wahanga wakuu wa matukio ya ubakwaji, ulawiti, utumikishwaji wa kazi za majumbani na vitendo vingine vya ukatili ikiwemo watoto wanaozunguka na kuombaomba mitaani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa KIWOHEDE Mama Mwaituka alisema wameridhishwa na jinsi wilaya inavyopambana katika kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsi na kwa kipindi chote walichofanya kazi Ikungi wameridhishwa na ushirikiano na namna halmashauri inavyotekeleza maelekezo ya kutokomeza vitendo hivyo japo bado jitihada zaidi zinahitajika katika kumaliza changamoto hiyo.
DC Muro alitumia nafasi hiyo kulishukuru shirika hilo kwa kuendelea kufanya kazi na wilaya hiyo hasa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na Timu yake kwa kuratibu jambo hilo kwa haraka na sasa wanakwenda kuongeza thamani katika kuwalinda watoto na wanawake katika Wilaya kwa mkakati na ubunifu mpya.