Home BUSINESS TUNDURU KUONGEZA UZALISHAJI KOROSHO KUTOKA KILO MILIONI 25 HADI KILO MILIONI 32...

TUNDURU KUONGEZA UZALISHAJI KOROSHO KUTOKA KILO MILIONI 25 HADI KILO MILIONI 32 MSIMU 2022/2023

Mwenyekiti swa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa kawaida wa 19 wa Chama Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu)uliofanyika katika Ukumbi wa Skay Way mjini Tunduru.
Baadhi ya wawakilishi wa taasisi za fedha zinazofanya kazi zake wilayani Tunduru wakiwa kwenye mkutano huo.
Baadhi ya Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Tunduru wakifuatilia taarifa mbalimbali za utekelezaji wa Chama hicho.

Na: Muhidin Amri, Tunduru.

CHAMA Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru(TAMCU LTD)kimepanga kuongeza uzalishaji wa zao la korosho kutoka kilo milioni 25,284,493 za msimu wa mwaka 2021/2022 hadi kilo milioni 32,000,000 katika msimu 2022/2023.

Hayo yamesemwa jana na Meneja Mkuu wa  Tamcu Imani Kalembo, wakati akitoa taarifa za maandalizi ya msimu mpya wa korosho  kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu  wa kawaida wa 19 wa Chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa Skay Way mjini Tunduru.

Alisema,katika msimu wa 2021/2022 Tamcu iliweka malengo ya kukusanya  na kuuza  korosho kilo milioni 25,lakini ilikusanya na kuuza kilo 25,284,493 zenye thamani ya Sh.bilioni 50,471,797,263.00 na hivyo kuvuka malengo kwa asilimia 101.14.

Akizungumzia zao la mbaazi alisema, katika msimu 2021/2022  zao hilo kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo minada sita ilifanyika na jumla  kilo milioni 4,111,845 zenye thamani ya Sh.bilioni 5,235,425,002.00 ziliuzwa.

Alisema,uzalishaji wa mbaazi  uliongezeka kutoka kilo milioni  2,206,296  za msimu 2020/2021 hadi  kilo 4,111,845 za msimu 2021/2022,hata hivyo  katika msimu 2022/2023 wamepanga kuongeza uzalishaji wa kilo 5,451,000.

Alisema,ongezeko la uzalishaji  wa mbaazi katika msimu wa 2021/2022 ulipanda kwa asilimia 186.37 na bei kwa kilo moja ilikuwa Sh.1,000 hadi 1,428 ikilinganisha na msimu 2020/2021 ambapo kilo milioni 2,111,845 tu zilikusanywa na kuuzwa kwa bei kati ya Sh.400 na 790.

Kwa upande wa zao la ufuta alisema,ulinunuliwa kwa  mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo jumla ya minada tisa ilifanyika na kilo milioni 2,219,283 zenye thamani ya Sh.bilioni 5,313,950,046.0 zilikusanywa na kuuzwa katika minada hiyo.

Hata hivyo alisema, uzalishaji wa ufuta ulishuka kutoka kilo 4,590,149 za msimu 2020/2021 hadi kufikia kilo 2,219,283 katika msimu 2021/2022 lakini bei ilikuwa kubwa kati ya Sh. Sh.2,204.91 na 2,393.00 ikilinganishwa na bei ya msimu 2021/2022 ambayo ilikuwa Sh.1,516.24 na Sh.2,240.25.

Mwenyekiti wa Tamcu Mussa Manjaule alisema,mkakati uliopo kama chama kikuu ni kuona mkoa wa Ruvuma unaongoza kwa uzalishaji wa zao la korosho hapa nchini kwa kuwa uwezo huo upo kutokana na mazingira mazuri.

Amewapongeza viongozi wa Amcos, kwa kazi nzuri wanayofanya kusimamia na kuendeleza sekta ya ushirika ambayo ina mchango mkubwa katika uzalishaji wa zao la korosho katika wilaya hiyo.

Naye mjumbe wa Bodi ya Korosho TanzaniaTanzania Faith Mitambo,amewapongeza wakulima wa zao la korosho wanaosimamiwa na TAMCU kwa kuvuka malengo ya uzalishaji wa  zao hilo katika msimu 2021/2022.

Alisema,wakulima wa korosho wanaohudumiwa na Chama hicho wameendelea kufanya vizuri kwa kuongeza uzalishaji  kutoka kilo milioni 15,000 msimu wa kilimo 2020/2021 hadi  kilo milioni 25,284,493 katika msimu wa 2021/2022.

Naye  Mwenyekiti wa wadau wa zao la Korosho Tanzania Rashid  Yusuph Nanila,amevipongeza vyama vya msingi vya Ushirika(Amcos)wilayani humo kwa kuendelea kusimamia vizuri suala la ushirika na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Alisema,uzalishaji wa zao hilo katika wilaya ya Tunduru unazidi kuongezeka  mwaka hadi mwaka, hata hivyo amewataka wakulima kuendelea kupanua mashamba yao  kwa kuwa katika wilaya hiyo kuna maeneo  makubwa na ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo cha korosho.

Pia amezitaka taasisi za fedha hapa nchini, kuharakisha  kutoa mikopo kwa wakulima ili  watumie kwenye mandalizi ya kilimo, kwa kufanya palizi na kununua pembejeo,badala ya kutoa wakati msimu wa maandalizi umekwisha.

Kwa mujibu wa Nanila ambaye ni  Rais wa Heshima wa zao la Korosho nchini, mashamba ya korosho yanaanza kufanyiwa palizi kati ya mwezi Februari na Machi,lakini hadi sasa hakuna taasisi ya fedha iliyotoa mikopo kwa wakulima jambo linaloweza kushusha uzalishaji kwa msimu wa 2022/2023.

Amewaasa viongozi wa Amcos kudumisha umoja na kushirikiana na Chama Kikuu cha Ushirika(Tamcu)katika majukumu yao ili kwa pamoja waweze kuwatendea haki wakulima.

Katika hatua nyingine, Nanila amemuagiza Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa ni Ruvuma,kutoa elimu ya ushirika kwa wanachama wa vyama vya msingi ili wafahamu ushirika jambo litakalo wezesha kuepusha migogoro katika vyama hivyo.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Julius Mtatiro ameipongeza Serikali kupitia wizara ya kilimo kwa kutoa Viuatilifu na pembejeo kwa wakulima bure,hatua iliyowezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo.

Mtatiro ametoa siku tatu kwa taasisi za fedha katika wilaya hiyo, kupeleka taarifa na takwimu za wakulima waliopewa mikopo ya pembejeo  na fedha kwa ajili ya shughuli za kilimo cha zao la korosho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here