Home LOCAL KONGAMANO LA KISAYANSI SEKTA YA MAJI LAFANA JIJINI DAR

KONGAMANO LA KISAYANSI SEKTA YA MAJI LAFANA JIJINI DAR

Naibu Waziri wa maji Mhe.Maryprisca Mahundi (Mb) (wapili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Meneja Mawasiliano wa DAWASA Bi. Everlasting Lyaroalipotembelea Banda la Taasisi hiyo mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kufungua Kongamano hilo.


Mwenyekiti wa Mameneja Mamlaka za Maji Vijijini Erwin Singisa (wa pili kulia) akiwa na Meneja wa RUWASA Morogoro John Msengi (wa kwanza kulia) wakipata maelezo kutoka kuhusu mradi wa utunzaji mazingira kutoka kwa Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Manispaa ya Shinyanga Angel Mwaipopo katika kongamano hilo.

DAR ES SALAAM.

Wadau wa Sekta ya Maji wamekutana jijini Dar es Salaam katika kongamano la Kisayansi lililowaleta pamoja wadau na watafiti mbalimbali katika sekta hiyo kujadili kwa mapoja tafiti zitakazoleta matokeo chanya katika rasilimali za maji.

Akifungua kongamano hilo, Naibu Waziri wa maji Mhe.Maryprisca Mahundi (Mb) amesema lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wadau wa sekta ya maji kujadili kwa pamoja tafiti mbalimbali zilizofanyika na zitakazoleta matokeo chanya katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.

“Kongamano hili ni muhimu sana katika kuandaa sera zetu za uendelezaji wa rasilimali maji lakini pia kuangalia uwezekano wa kutumia ili kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za usimamizi wa rasilimali hizi” aliongeza Mhe Mahundi

kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Maji, Dkt Adam Karia ambao ni waandaaji wa kongamano hili alisema lengo la kuandaa kongamano hili ni kujadili na kuiboresha sekta ya maji kupitia wataalamu mbalimbali walionao na wanaoendelea kuingia katika sekta ya maji.

“Naishukuru Serikali kwa kuendelea kuthamini juhudi mbalimbali zinazotekelezwa na Chuo Cha Maji hususani katika kuandaa kongamano hili litakalowakutanisha wadau zaidi ya 400 kutoka sehemu mbalimbali ili kuendelea kuhakikisha changamoto katika sekta ya maji zinapatiwa ufumbuzi “ alisema Dkt Karia

Naye Meneja Mawasilianowa DAWASA Everlasting Lyaro amesema ushiriki wao kama Mamlaka ni kupata nafasi ya kujifunza na kupitia kwa kina tafiti zilizopitiwa ambazo zinaweza kutoa ufumbuzi wa changamoto katika sekta ya Majisafi na Usafi wa Mazingira.

“Sisi kama Mamlaka tunatumia nafasi hii kukutana na kusikiliza tafiti mbalimbali za wadau wa sekta ya Maji ili kuweza kupata ufumbuzi wa mambo mbalimbali yahusuyo huduma za maji. Ni wakati muafaka wa Serikali kuzipa kipaumbele tafiti hizi zilizoandikwa na wabobezi ili zikatoe majibu ya sera mbalimbali za sekta” alisema Lyaro. 

Kongamano hilo lenye kaulimbiu “Usimamizi wa Rasilimali za maji kwa huduma endelevu za usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira” linafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 04 na tarehe 05.April, 2022 huku Taasisi zaidi ya 20 zikishiriki.

Credit – Michuzi blog.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here