Home LOCAL WATUMISHI WIZARA YA HABARI WAJENGEWA UWEZO KUBAINISHA VIHATARISHI

WATUMISHI WIZARA YA HABARI WAJENGEWA UWEZO KUBAINISHA VIHATARISHI

Na Lilian Lundo – MAELEZO.

Watumishi wa wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kubaini vihatarishi katika maeneo yao ya kazi na kuchukua hatua ya kuvisimamia na kuvidhibiti. 

Mafunzo hayo yamefanyika leo, Februari 21, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa maktaba ya mkoa, Jijini Dodoma ambapo Mkurugenzi wa Utawala na Rasimali Watu wa Wizara ya Habari, Teddy Njau alifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi. 

“Mafunzo haya ni mwendelezo wa utekelezaji wa mpango wa usimamizi wa vihatarishi ulioandaliwa yaani Risk Management Framework ili kuwezesha kila mtumishi kuwa na uelewa wa vihatarisha kwenye eneo lake la kazi  na kuchukua hatua za kuvisimamia na kuvidhibiti,” alisema Teddy. 

Aliendelea kusema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kujenga uwezo kwa watumishi wote wa kila idara na kitengo katika kubaini vihatarishi vilivyopo na kuandaa mpango wa kuvifuatilia na kukabiliana navyo ili kupunguza athari zake au kuviondoa kabisa ili visikwamishe utekelezaji wa majukumu ya wizara ili kufikia malengo yanayokusudiwa. 

“Ni wazi kwamba kama sekta ya umma, tunatakiwa kusimamia na kudhibiti kwa umakini mkubwa vihatarishi ambavyo vipo na vinaweza kutokea muda wowote na mahali popote tunapotekeleza majukumu yetu ya kila siku katika ngazi zote,” alifafanua Teddy. 

Aidha ametaja majukumu hayo yanayotekelezwa na Wizara ya Habari, kuwa ni pamoja na utungaji, usimamizi na utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na miongozo inayohusu sekta ya Habari na Mawasiliano ikiwemo miundombinu ya TEHAMA na huduma za mawasiliano pamoja na mazingira ya kila siku ya kazi. 

Kwa upande wake, Afisa Habari wa Idara ya Habari, Daudi Manongi, amesema mafunzo hayo yamempa mwanga wa kubaini vihatarishi katika kazi zake za kila siku. 

“Ni mara yangu ya kwanza kupata mafunzo haya, nilikuwa nafanya kazi bila kutambua vihatarishi ambavyo vipo katika kazi ninazozifanya, jambo ambalo lilikuwa si salama  katika utekelezaji wa majukumu yangu ya kila siku,” alifafanua Manongi. 

Aliendelea kusema kuwa, mafunzo hayo yamemsaidia kutambua vihatarishi vilivyopo katika majukumu yake ya kila siku hivyo kumsaidia kukabiliana navyo au kuviondoa kabisa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here