Na: Georgina Misama – Maelezo, 26/02/2022
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi amesema Serikali imefanya juhudi kubwa kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano nchini ambapo mpaka sasa idadi kubwa ya Watanzania wamefikiwa na huduma hiyo.
Akizungumza katika mdahalo maalumu uliohusu masuala ya ubunifu na teknolojia kwa vijana uliyofanyika jijini Dar es Salaam Februari 25, 2022 Dkt. Yonazi alisema Serikali inafanya mambo mengi katika kuwekeza kwenye miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
“Kati ya juhudi zilizofanywa na Serikali katika kuwekeza kwenye miundombinu ya mawasiliano ni pamoja na mitandao ya simu ambapo mpaka hivi sasa tumewafikia asilimia 94 ya Watanzania wote, asilimia 66 ya maeneo yamefikiwa na namba ya watumiaji wa internet imeongezeka kutoka milioni 5 mwaka 2010 mpaka milioni 29.8 mwaka 2021”alisema Dk. Yonazi.
Aliongeza kwamba bado serikali inaweka nguvu katika kufikia baadhi ya maeneo ambayo hayajafikiwa hasa ya vijijini na maeneo ya mipakani ili kuwafikia Watanzania wote hasa wakati huu ambao msisitizo mkubwa upo katika kuifanya Tanzania kuwa kituo cha TEHAMA.
“Hivi sasa tuna mradi mkubwa unaoendelea unaoitwa ‘Digital Tanzania’ lengo kubwa la mradi huo ni kuifanya Tanzania kuwa kituo cha TEHAMA ambapo katika eneo la wataalam tunahitaji tuwe nao wa kutosha wawe na ujuzi sahihi na wapatikane na kuunganishwa kwa urahisi” aliongeza.
Dkt. Yonazi alitoa pongezi kwa waandaji wa mdahalo huo na kuwashukuru kwani amepata nafasi ya kusikiliza mawazo ya vijana kuhusu sekta anayoiongoza na kutoa ushauri kwa waandaji mdahalo huo, kwamba watakapoandaa tena mdahalo kama huo, wawaalika wataalam wa sayansi ambao watasaidia kutoa mwongozo kwa Serikali kwa kuweka mbinu bora na endelevu kwa maendeleo ya Taifa.
Mdahalo huo uliandaliwa na taasisi ya Media Convergency, ambapo ulihudhuriwa na vijana pamoja na makundi mbalimbali ya wadau wa masuala ya TEHAMA, ambapo kauli mbiu iliyoongoza mdahalo huo ni Mazingira Wezeshi kwa Vijana na Wanawake Kuelekea Uvumbuzi wa Kibiashara
MWISHO.