Mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Taasisi ya Be all trust fund,Jumaa Mwaipopo ameiomba Serikali kuwatafutia maeneo ya kufanyia biashara wamama wajane kwa kuwa wamebaki kuwa ombaomba na kukata tamaa baada ya kuondolewa kufanya biashara pembezoni mwa barabara.
Kauli hiyo imetolewa na Mwaipopo alipokuwa akitoa msaada wa vyakula mbalimbali ikiwemo mchele kwa ajili ya sikukuu ya mwaka mpya kwa wajane pamoja na wagonjwa walio majumbani.
Amesema kutokana na zoezi la serikali kuwaondoa wafanyabiashara barabarani limewaathiri wajane hao ambao walikuwa wanafanya biashara zao kutokana na mikopo ikiwemo ya vikoba na taasisi za kifedha ambapo waliweza kuwasomesha watoto wao lakini Kwa sasa wanashindwa kurudisha mikopo hiyo na kubaki kuwa ombaomba huku wakikata tamaa.
“Kwani biashara walizokuwa wanafanya ziliwapa matumaini japo kidogo walikuwa wakiwasomesha watoto wao lakini sasa hivi wanashindwa kurudisha mikopo sasa hivi wamekuwa ombaomba,”alisema Mwaipopo.
Amesema kuwa taasisi hiyo inajishugulisha na wajane, yatima, waathirika na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ambapo walipata maombi kuwa kuna wagonjwa wa muda mrefu wapo majumbani wamekata tamaa kutumia dawa kutokana na njaa Jambo ambalo linawafanya wachanganyikiwe.
Mwaipopo alisema kutokana na hilo ametoa vyakula ikiwemo mchele kwa wagojwa wa majumbani pamoja na wajane hivyo aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia chakula.
Amesema taasisi hiyo inawahudumia wajane hao lakini haina uwezo hivyo wdadau mbalimbali wajitokeze kuwasaidia chakula kwani baadhi yao wanalala na njaa huku wengine wagonjwa wanashindwa kutumia dawa kutokana na njaa.
Kwa upande wa Imamu wa msikiti wa Ukonga Magereza,Abdalah Shiba alisema inayowazunguuka hao wajane inawajibu wa kuwaangalia Kwa kuwa uislamu unahimiza kuwatunza na kuwaangalia kama kundi muhimu linalohitajika.
Naye mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Tanzani(KLPT),Amani Mnyuke alisema watu wenye uwezo wapo wengi lakini inapofika kwenye suala la kusaidia wamekuwa wakijitokeza wachache.
“Nawaomba wajitokeze kuwasaidia wajane wanapotoa Mungu anawaongezea pale walipotoa,”alisema Mnyuke.
Naye mmoja wa wajane hao Flora Chipatikila alisema taasisi hiyo imekuwa ikiwasaidia tangu mwaka 2010 hivyo ameishukuru na kuwaomba watu na wadau mbalimbali waige mfano hio Kwa kuwasaidia wajane hao.
Mwisho