Home LOCAL TCB YATOA MSAADA WA SARUJI SHULE YA MSINGI MCHENGAMOTO

TCB YATOA MSAADA WA SARUJI SHULE YA MSINGI MCHENGAMOTO

Wanafunzi wa Darasa la sita shule ya msingi Mchengamoto kata ya Namasakata Jimbo la Tunduru Kusini wakiwa wamekaa dawati moja wanafunzi watano kama wanavyoonekana katika darasa ambalo halijapigwa lipu wala sakafu jambo linalowaathiri sana kimasomo, hata hivyo Benki ya TCB Tawi la Tunduru limetoa msaada wa mifuko 60 ya saruji kwa ajili ya kukarabati vyumba viwili vya madarasa.

Na: Muhidin Amri,Tunduru

BENKI ya Biashara Tanzania(TCB)imetoa mifuko 60 y saruji yenye thamani ya Sh.930,000 katika shule ya msingi Mchengamoto kata ya Namasakata wilayani Tunduru ili kuunga mkono juhudi za wananchi na serikali za kuimarisha miundombinu ya shule.

Akizungumza wakati wa kukabidhi saruji hiyo,Kaimu Meneja wa Benki ya TCB wilayani Tunduru  Chacha Petro alisema, TCB imekuwa inatoa msaada wa fedha na vifaa mbalimbali kila mwaka kama sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii inayowazunguka kulingana na mahitaji ya jamii husika.

Alisema, lengo la kutoa msaada huo wa saruji ni kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za wananchi na serikali kupitia Halmashauri ya wilaya ya Tunduru za kuimarisha na kuboresha  sekta ya elimu ambayo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Alisema,TCB imelazimika kuungana na serikali ya awamu ya sita kwa kutoa mifuko hiyo ya saruji kwa ajili ya kukarabati vyumba viwili vya madarasa kutokana na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi wa shule hiyo.

“lengo la Benki ya TCB kuhakikisha watoto wetu wanakuwa na sehemu nzuri ya kujisomea ili waweze kutumiza ndoto zao,mtoto hawezi kusoma vizuri iwapo hakuna mazingira mazuri na miundombinu bora hivyo sisi kama wadau  wa elimu tumeona tuna wajibu wa kusaidia”alisema Chacha.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Mchengamoto Francis Msumba,ameipongeza Benki  ya TCB  kwa namna ilivyoguswa katika kuchangia shule hiyo ambayo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa,madawati na walimu.

Msumba alisema, msaada huo wa saruji utakuwa chachu kwa wanafunzi kusoma kwa bidii kwani watapata sehenzu nzuri ya kujisomea na utahamasisha wananchi wa kijiji hicho kujitokeza kusaidia nguvu zao katika ujenzi wa vyumba vya madarasa na miundombinu mingine.

Alisema, kwa sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 243 wanaotumia  vyumba saba vya madarasa  kati ya hivyo viwili havijapigwa lipu  wala sakafu na havitoshi kulingana na  idadi kubwa ya wanafunzi 243 waliopo katika shule hiyo.

Alisema mbali na changamoto ya madarasa,shule hiyo  ina upungufu mkubwa wa madawati kwani mahitaji ni madawati 90 na yaliyopo ni 35, hivyo kuwa na upungufu wa madawati 55 jambo linalowalazimu wanafunzi  kukaa 5 hadi 6 katika dawati 1.

Diwani wa kata ya Namasakata Rashid Husanje, amempongeza Mwalimu Mkuu na kamati ya shule kwa ubunifu wao kutafuta wadau kwa ajili ya kupungufu baadhi ya changamoto zinazoikabili shule hiyo badala ya kuisubiri Serikali.

Husanje amewataka wazazi,walezi na jamii inayozunguka shule hiyo, kujitolea nguvu na fedha ili kwa pamoja  waweze kumaliza tatizo la miundombinu ya elimu na watoto wapate sehemu sahihi ya kusoma.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa wilaya hiyo  Joshua John ameishukuru Benki ya TCB kwa msaada huo ambao unakwenda kutumika kuimarisha  na kuboresha mazingira ya kujifunza kwa wanafunzi na kufundishia kwa walimu.

Amezitaka taasisi nyingine zilizopo ndani na nje ya wilaya hiyo, kujitokeza kutoa sehemu ya faida wanazopata kupeleka faida kwa jamii ili kuboresha utendaji kazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Amewaomba wananchi, kuwa mstari wa mbele kujitolea nguvu katika ujenzi wa madarasa na miradi mbalimbali  inayojengwa na Serikali kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji kazi  kwa watumishi na kuharakisha maendeleo badala ya kuichia serikali.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji Andrea Namagono alisema,wananchi wa kijiji hicho wameshatoa mbao 100 kwa ajili ya kutengeneza madawati na meza  ili kukabiliana na upungufu wa madawati kwa wanafunzi.

Kwa  upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Chiza Malandu alisema, hali ya miundombinu ya elimu katika wilaya ya Tunduru ni tatizo kubwa kutokana na  changamoto ya fedha  ambapo wanahitaji zaidi ya Sh.bilioni 13.
MWISHO.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here