Na: WAMJW-DSM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima leo Desemba 6, 2021 amefanya ziara ya kushtukiza ili kujionea hatua mbalimbali zinazochukuliwa na wananchi pamoja na viongozi katika kupambana na kudhibiti maambukizi ya UVIKO-19 katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi Jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo Dkt. Gwajima amebaini bado utekelezaji wa Miongozo ya Kujikinga dhidi ya UVIKO-19 haifuatwi hivyo jamii kujiweka katika hatari zaidi za kujikinga dhidi ya Wimbi la Nne la Ugonjwa wa UVIKO-19.
Amesema, ni muhimu kila Mamlaka ya Utawala ngazi zote na maeneo yote hadi katika kituo hiki cha mabasi kujitoa kwa nafasi yake katika mapambano haya dhidi ya UVIKO-19, hasa ukizingatia hili ndio lango kuu la wananchi kutoka sehemu mbali mbali kufika katika Jiji la Dar es Salaam na wengine kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa yote Tanzania Bara.
“Hapa ndiyo lango la abiria wanaotoka na kuingia ndani ya Dar es Salaam, hivyo inaonekana zoezi la unawaji mikono haliridhishi na maji yaliyopo ni machache hivyo kufanya unawaji usiwe wa ufanisi” Amesema Dkt. Gwajima.
Aidha, ametoa wito kwa Wadau wanaounga mkono jitihada za Serikali za kupambana dhidi ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa UVIKO-19 kuchangia maboresho katika kituo hicho ili kusaidia wananchi wanaofika kupata huduma za usafiri kuwa salama.
Kwa upande mwingine Amesema, bado afua ya uvaaji barakoa imekuwa haifuatwi kwa kiasi kikubwa, hali inayohatarisha wananchi wanaofika katika kituo hicho kupata huduma mbalimbali ikiwemo huduma ya usafiri.
“Sielewi kwa nini mnashindwa kuelimisha wananchi na kuweka utaratibu kuwa kila mmoja anayeingia hapa awe amevaa barakoa na amenawa mikono na kama amesahau barakoa basi uwekwe utaratibu mzuri wa kuuza barakoa za MSD au Muhimbili zinazouzwa bei nafuu ili kusaidia kuwakinga wananchi ” Amesema.
Kwa upande mwingine Dkt. Gwajima amesema, bado Chanjo ni hiari kwa kila mwananchi lakini Serikali itaendelea kutoa Elimu ya kutosha kwa wananchi ili kuhakikisha wanauona umuhimu wa kuchanja na wanahamasika kuchanja na kuepuka kuingia katika oksijeni na mwishowe kifo.
“Chanjo bado ni hiari, lakini chanjo ni muhimu walio na neema kubwa zaidi ya kuukwepa UVIKO-19, ni waliochanja na wasiochanja hawana neema kubwa na ndiyo hao wanaoingia kwenye oksijeni na wengi wao hupoteza maisha” Amesema.
Ameendelea kusema kuwa, ni muhimu kuendelea kuwakumbusha wananchi afua zote za kupambana dhidi ya UVIKO-19 kupitia afua ya chanjo na za unawaji mikono, uvaaji barakoa na kujiepusha na misongamano isiyo ya lazima.
Mbali na hayo amesema, nchi inaelekea kwenye kipindi cha mvua za masika hivyo ni muhimu kujiandaa kujikinga dhidi ya magonjwa ya msimu wa mvua.
Aidha, amewaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kutoka ofisini na kwenda kutoa elimu ya kutosha kwa viongozi wengine na jamii ili nao wachukue wajibu wa kwenda kwa wananchi kuelimisha na kuhamasisha huku akisisitiza wakae na Wadau katika maeneo yao ili kujiimarisha namna ya kupambana dhidi ya UVIKO-19 na magonjwa mengine ya msimu huu wa mvua za masika.
Mwisho.