Home LOCAL WAZIRI NDAKI AKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA OMAN

WAZIRI NDAKI AKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA OMAN


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya Desert Cold Store kutoka Oman, Dkt. Munawar Pardhan  alipokutana na Wawekezaji kutoka nchini Oman jijini Dar es Salaam. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati) akibadilishana mawazo na sehemu ya Wawekezaji waliomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam Novemba 26, 2021. Kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Desert Cold Store kutoka Oman, Dkt. Munawar Pardhan
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wawekezaji kutoka nchini Oman muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika  jijini Dar es Salaam Novemba 26, 2021. Wengine ni Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

 Na:Mbaraka Kambona,

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema Wizara yake itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayowavutia wawekezaji katika Sekta ya Mifugo ili kukuza thamani ya mifugo na kupandisha kipato cha wafugaji hapa nchini.

Ndaki aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana alipokutana na Wawekezaji kutoka nchini Oman ambao wameonesha nia ya kufanyabiashara ya  kununua mifugo na nyama hapa nchini na kuuza nchini Oman.

“Tunaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kadri iwezekanavyo ili muweze kufanya hiyo biashara na nchi yetu,” Mhe. Ndaki aliwaeleza wawekezaji hao.

Alisema kuwa nchi ikipata wawekezaji kutoka nje kama wao ni jambo jema kwa sababu kupitia wao wafugaji watapata kipato kizuri,  lakini pia itapandisha thamani ya mifugo nchini.

“Tukipata soko la kwenu litasababisha wafugaji wetu ambao wengi wao kipato chao kipo chini kiweze kupanda, sisi tutafanya kila linalowezekana ili biashara hii mnayotaka kuifanya iweze kufanikiwa,” alisistiza.

Awali, Mkurugenzi wa Kampuni ya Desert Cold Store kutoka Oman, Dkt. Munawar Pardhan alisema lengo lao ni kufanya biashara ya mifugo na nyama, huku akisema kuwa wakifanikiwa itakuwa ni fursa kubwa ya kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

“Tumekuja hapa Tanzania kujua taratibu za kufuata ili tuweze kufanya biashara ya mifugo na nyama kutoka hapa na kwenda kuuza nchini Oman,” alifafanua

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here