Home LOCAL WASICHANA WAHAMASISHWA KUJIUNGA MAFUNZO YA UFUNDI STADI.

WASICHANA WAHAMASISHWA KUJIUNGA MAFUNZO YA UFUNDI STADI.

Na: Lucas Raphael,Tabora

VIJANA wa Jinsia ya Kike Mkoani Tabora wametakiwa kuchangamkia fursa za Mafunzo ya Ufundi Stadi zinazotolewa katika Chuo Cha VETA ili kupata ujuzi utakaowawezesha kujipatia kipato. 

Ushauri huo umetolewa jana na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Magharibi Asanterabi Kanza katika sherehe za mahafali ya 23 ya wanafunzi wa Chuo hicho Mkoani hapa. 

Alisema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1999 hadi sasa vijana wa kiume wamekuwa wakijitokeza kwa wingi zaidi kujiunga na mafunzo hayo na kunufaika tofauti na wenzao wa kike. 

Akibainisha kuwa serikali imekuwa ikitoa fursa mbalimbali kwa vijana wa kiume na kike kujiunga na mafunzo ya stadi mbalimbali za maisha ili kupata ujuzi utakaowainua kiuchumi lakini mwitikio kwa akinadada umekuwa si wa kuridhisha.

Kanza alisisitiza kuwa VETA ni mkombozi kwa vijana kwani huwapa maarifa na ujuzi wa shughuli ambazo zinaweza kuwaingia fedha hivyo kujikwamua kimaisha na sio kuendelea kutegemea wazazi au marafiki. 

Aliongeza kuwa vijana wanaohitimu mafunzo ya Ufundi Stadi katika Vyuo vya VETA wana nafasi kubwa kupata ajira rasmi au zisizo rasmi kwa kuwa wamepata mafunzo ya nadharia na vitendo na wana uwezo mkubwa katika fani zao. 

Alitoa mfano wa wahitimu 153 wa mwaka huu katika Chuo Cha VETA Tabora kuwa wanaume ni 102 na wanawake 51 tu jambo linaloonesha mwitikio wa vijana wa kike kujiunga na mafunzo hayo bado ni mdogo licha ya manufaa wanayopata.

‘Wazazi hamasisheni watoto wenu wa kiume na kike kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi ili wapate ujuzi wa fani mbalimbali zitakazowasaidia kujiajiri wenyewe na sio kusubiri ajira za serikali’, alisema. 

Aidha aliomba taasisi mbalimbali za umma na binafsi kuwapa nafasi za kufanyia mazoezi ya vitendo wahitimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi ili kuwaongezea ujuzi wa fani zao na wakiona wanafanya vizuri zaidi wawaajiri moja kwa moja.

Awali Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Japhary Mwambete alisema chuo hicho kilianza mwaka 1999 kikiwa na fani 3 tu za useremala, useketaji na komputa lakini sasa kina kozi zaidi ya 10 na serikali imeendelea kufadhili vijana zaidi kuja kujifunza fani mbalimbali ili kuwawezesha kupata ujuzi wa stadi za kazi. 

Alibainisha baadhi ya mipango ya Chuo hicho kuwa ni kuongeza idadi ya fani ili kwendana na soko la ajira, kuongeza mabweni, kuboresha karakana na kuweka vifaa vya kisasa na kuboresha huduma za hosteli ikiwemo kuanzisha hoteli chuoni.

Mwisho.

Previous articleDKT. GWAJIMA AWATAKA WALIMU KUSIMAMIA NIDHAMU
Next articleRAIS MUSEVEN AWASILI NCHINI KUANZA ZIARA YA KISERIKALI YA SIKU TATU
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here