Home LOCAL WALIOFELI, WALIOPATA MIMBA RUKSA KURUDI SHULE: RAIS SAMIA

WALIOFELI, WALIOPATA MIMBA RUKSA KURUDI SHULE: RAIS SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni akimkabidhi mfano wa funguo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kama ishara ya makabidhiano ya Shule hiyo ya Awali mara baada ya uzinduzi uliofanyika katika Shule hiyo ya Museveni Pre & Primary School Chato mkoani Geita

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni kwa pamoja wakikata utepe kuzindua rasmi Shule ya Awali na Msingi Museveni Pre & Primary School iliyojengwa kwa msaada wa Rais Yoweri Museveni Wilayani Chato Mkoani Geita.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni kwa pamoja wakiondoa kitambaa  kuzindua rasmi Shule ya Awali na Msingi Museveni Pre & Primary School  iliyojengwa kwa msaada wa Rais  Yoweri Museveni Wilayani Chato Mkoani Geita. (PICHA NA: IKULU).

Na: Georgina Misama – MAELEZO, 29/11/2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeamua kuwapa nafasi ya pili wanafunzi wote wa shule za msingi nchini ambao walipata changaoto mbalimbali zilizowakwamisha kuendelea na masomo yao ikiwemo mimba, utoro na kufeli mtihani wa darasa la saba kurudi shule kwaajili ya kusoma na kufanya tena mtihani huo.

Rais Samia alisema kwamba uzoefu unaonyesha kwamba kundi la watoto wa kike wanaoshindwa shule ya msingi sababu ya kupata ujauzito huwa hawaendelei na masomo hata baada ya kujifungua tofauti na wale wa sekondari ambao wengi wao hurudi na kuendelea na masomo yao mpaka ngazi za juu za elimu.

Akiongea leo Novemba 29, 2021 katika hafla ya makabidhiano ya Shule ya Msingi na Awali  Museveni iliyopo Kijiji cha Nyabilezi, Wilayani Chato mkoa wa Geita,akiwa na mgeni wake  Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museni ambaye pia ni mdhami wa ujenzi wa shule hiyo , Rais Samia alisema kwamba Serikali imeamua kutoa fursa ya kuwarudisha shule wanafunzi wote walioacha na kufeli ili kuhakikisha watoto wa kitanzania wanajikwamua kielimu.

“Tumeamua watoto wote ambao waliacha shule kwa sababu mbalimbali na wale waliodondoka kwenye mtihani wa darasa la saba tuwape nafasi nyingine ya kurudi shule na kufanya tena mtihani huo, kwa wale ambao wanaona hawawezi kurudi tena shule tumewawekea mpango mwingine unaitwa elimu mbadala ‘altenative education’ watakwenda kwenye mkondo huo ili wakitoka hapo waweze kufanya miradi itakayowasaidia kujitunza”,alisema Rais Samia.

Aidha, aliongeza kuwa suala la kuwarudisha shule watoto wa kike walioacha sababu ya kupata ujauzito lisiwaletee mashaka  na kuwapotezea  muda Watanzania kwa kuanza kulijadili kwani Serikali imejipanga na imeona mifano kutoka kwenye nchi nyingine zinazofanya hivyo na kupata uhakika halitaleta uhalibifu wowote ndani ya mfumo wa elimu kutoka shule za msingi mpaka sekondari.

Akiongelea shule ya Museveni Rais Samia alimshukuru Rais Museveni kwa niaba ya Wanzania wote kwa utu na wema wake kwa ujenzi wa shule hiyo uligharimu zaidi ya  Dola za Kimarekani milioni 1 kwani ametambua kwamba suala la elimu bora halina mipaka bali ni jukumu la viongozi wote wa Afrika kuhakikisha kwamba wanatoa elimu bora na yenye viwango ili kuweza kukidhi soko la ajira.

“Makabidhiano ya shule hii yanafanyika wakati muafaka, kipindi ambacho Serikali inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Elimu ya Msingi bila Ada ambapo shule hii italeta manufaa ya kutengeneza fursa kwa wanafunzi wote kupata elimu kwenye majengo haya ambayo yamezingatia pia wanafunzi wenye uhitaji maalumu lakini pia itaimarisha utoji wa elimu bora kwa uwepo wa miundombinu yote muhimu” aliongeza.

Rais Samia aliiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi yenye dhamana kuandaa historia ya shule hiyo na kuiweka kwenye maktaba shuleni hapo ili watoto  watakaosoma shule hiyo waijue na kuienzi  pamoja na kuweka kumbukumbu za uhusiano mzuri na wa kindugu uliopo kati ya Tanzania na Uganda. 

Kwa upande  wake Rais Museveni alisema kwamba alifanya uamuzi wa kujenga shule hiyo kutokana na sababu za kindugu na uhusiano wake na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufuli ambaye walikubaliana ajenge shule kijijini hapo alipokwenda kumtembelea enzi za uhai wake.

“ Marehemu hakuniomba wala hakuniagiza bali nilipokuja hapa mara ya mwisho alipendekeza tujenge shule hapa na tuiite jina la Museveni, sikujua kwanini aliniambia hivyo ila nadhani ni kwasasabu alijua nilifanya hivyo maeneo mengine hapa Tanzania”,alisema Rais Museveni.

Aliongeza kuwa Mungu amemwekea Muafrika msingi mzuri wa kuelewana kwa lugha, ambapo ikiwa utatumika vizuri kibiashara itakuwa mkombozi kiuchumi. Aidha, aliongelea faida ya mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Ohima Uganda mpaka Chongoliani Tanga ambapo mkoa wa Geita unapitiwa na mradia huo aliwataka wakazi wa Chato kutumia fursa hiyo ili iwakomboe kiuchumi.

“Kuhusu faida za ujenzi wa bomba la mafuta, nawasihi msiwe watu wa kufanyia tumbo pekee, Serikali haiwezi kuwafanyia kila kitu, haiwezi kuwajengea nyumba wala kuwanunulia mahitaji mengine na nchi haiwezi kuendelea kwa namna hiyo, mkilima mtauza chakula, msipolima watakaofanya kazi katika mradi huo watanunua chakula kutoka nje”alisisitiza.

Hafla ya makabidhiano ya Shule ya Museveni ilihitimisha ziara ya siku tatu ya Rais Museni hapa nchini, ambapo kabla ya hapo alishiriki kwenye kongamano la kibiashara lililofanyika Ikulu  Jijini Dar es Salaam pamoja na kutembelea mradi wa SGR.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here