Home LOCAL SULTANI MATAKA WA WAYAO NA VIONGOZI WA JADI WAFANYA MAOMBI YA KULIOMBEA...

SULTANI MATAKA WA WAYAO NA VIONGOZI WA JADI WAFANYA MAOMBI YA KULIOMBEA TAIFA

 Chifu wa kabila la Wangoni kutoka Songea Emmanuel Zulu aliyevaa mavazi rasmi ya Kichifu akiwaongoza baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kidodoma wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kwenda kuchanja chanjo ya Covid 19  baada ya kumalizika kwa maombi ya kuliombea Taifa kuhusu ugonjwa huo,kulia Diwani wa Kidodoma Shaban Nyenje.

Chifu wa kabila la Wangoni kutoka Songea Emmanuel Zulu Gama kulia akitoa damu jana kwa ajili ya kupima afya wakati wa kampeni ya uibuaji wa ugonjwa wa kifua kikuu katika kijiji cha Kidodoma wilaya ya Tunduru, kushoto ni mtaalam wa maabara kutoka shirika lisilo la kiserikali ya MDH Anna Enock


Muuguzi wa Zahanati ya Kidodoma wilaya ya Tunduru Elice Makumbuli akitoa chanjo ya Corona kwa mkazi wa kijiji hicho Yasin Tawala wakati wa zoezi la utoaji chanjo ya Uvico-19 linaloendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Na: Muhidin Amri,Tunduru

KIONGOZI wa kabila la Wayao wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Said Mussa (Sultani Mataka) machifu na viongozi wa jadi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma wamekusanyika  katika kijiji cha Kidodoma wilayani humo kwa ajili ya kufanya maombi ya kuliombea Taifa kuhusu ugonjwa wa Covid-19.

Sultani Mataka alisema, wamelazimika kufanya maombi maalum kwa Mwenyezi Mungu ili ainusuru nchi yetu na ugonjwa huo ambao  unaendelea kupoteza maisha ya Watanzania wengi na kupunguza nguvu kazi ya Taifa.

Kiongozi huyo wa  kabila la Wayao, amewaomba Watanzania kuendelea  kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo na kujitokeza kwa wingi  kupata chanjo katika vituo vilivyotengwa na Serikali.

Aidha Sultani Mataka, amewataka wananchi kuzingatia maelekezo na ushauri unaotolewa na wataalam wa afya ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka,kuvaa barakoa na kutumia vitakasa mikono.

Alisema, kila mwaka wanafanya maombi ya kuliombea Taifa  kulingana na  tatizo lililopo  na  kabla ya maombi wanakwenda  kwenye makabauri ya  Mababu zao kwa ajili ya kupata baraka ambazo kwa imani za kabila la Wayao  zinasaidia kufanikisha mahitaji na shida zao.

Mwenyekiti wa viongozi wa jadi wa wilaya ya Tunduru Issa  Malungusya alisema, kila mwaka Sultani,Machifu  na viongozi wa jadi wanakutana nyumbani kwa Sultani Mataka kwa ajili ya maombi  maalum  kuhusiana na  shida na jambo lililo mbele yao ili Mwenyezi Mungu aweze kuwanusuru.

Alisema, kwa sasa hali ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo hapa nchini  sio nzuri licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali,hivyo  wana amini mwenye uwezo wa kumaliza tatizo la Corona ni Mungu.

Amewataka wananchi hasa wakazi wa wilaya ya Tunduru,  kuendeleza mira na utamaduni  wa kabila  lao kwani hatua hiyo inasaidia sana kupunguza  na hata kutokomeza baadhi ya majanga yanayojitokeza katika jamii  badala ya kukumbatia utamaduni kutoka nje.

Naye Chifu wa  kabila la Wangoni  kutoka Songea Emmanuel Zulu  Gama amefurahi kushiriki katika maombi hayo ili kwa pamoja  wamuombe Mungu aweze  kuisaidia Nchi yetu kutokomeza ugonjwa huo ambao unaendelea  kupoteza maisha ya wananchi wengi

Chifu Zulu Gama,amewaomba Watanzania kujithamini  na kuwa waangalifu kwa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo na magonjwa mengine na kuepuka tabia ya kupuuza ushauri unaotolewa na wataalam wa Afya.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Tunduru Dkt Wendy Robert alisema,mwitikio wa Wananchi kujitokeza kupata chanjo ya Corona ni mkubwa na  kusisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya afya itaendelea kupeleka chanjo katika maeneo yote.

Amewataka wananchi wa wilaya hiyo,kuchangamkia kupata chanjo na kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya zao mara  kwa mara ili kuwa na uhakika wa afya zao.

Kwa mujibu wa Dkt Wendy,wilaya ya Tunduru imejipanga kuhakikisha maeneo yote yanakuwa na chanjo za kutosha na hakuna mwananchi atakayekosa huduma hiyo ambayo inatolewa bure na wahudumu wa afya.
MWISHO

Picha zote na Muhidin Amri,

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here