Kamishna wa polisi jamii kutoka jeshi la polisi Tanzania Dkt Musa Ali Musa akiongea na waandishi wa habari mkoani Arusha katika mkutano wa makamisha na makamanda wa polisi nchini.
Naibu Balozi wa Ireland Mags Gaynor akiongea na waandishi wa habari mkoani Arusha katika mkutano wa makamisha na makamanda wa polisi Tanzania mkutano uliofadhiliwa na ubalozi huo
NA: NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Kamishna wa polisi jamii kutoka jeshi la polisi nchini Dkt Musa Ali Musa amesema kuwa changamoto za Rushwa na tamaduni za jamii mbalimbali bado zinachangia uwepo wa makosa ya ukatili wa kingono ambapo ili kupambana na makosa hayo madawati jinsia yanapaswa kujikita katika kuandaaa programu ambazo zitaendana na taratibu za wananchi na changamoto walizonazo.
Dkt Musa aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa kitaifa wa makamishana wa polisi na makamanda wa polisi Tanzania juu ya upatikanaji wa haki jinai kwa watoto waathirika wa ukatili wa kingono ambapo alisema kuwa ni lazima wajikite katika kuandaaa programu ambazo hazitakuwa za kipekee kwani matatizo ya ukatili yanaenda mbali zaidi kutoka jamii moja hadi nyingine.
“Tunataka kupitia mkutano huu tuandae programu ambazo zitafiti katika jamii zote ambapo pia tuatangalia tatizo la vijana wengi wa Sasa kutokwenda shule kwani changamoto hii inachangia kuja kuwa na waalifu wa aina mbali mbalimbali na tukiweza kupambana nao huku chini itasaidia kuondokana nayo hapo baadae,” Alisema.
Alifafanua kuwa kwa kutumia madawati hayo na kulingana na wadau wengine kwenda mashuleni na kujua ambao hawahudhurii na kuweza kuwarudisha shule itaondoa tatizo kwa baade kwani matokeo ya kutokwenda shule yanasababishwa kuja kuwa na waalifu wa aina mbalimbali ikiwemo hayo ya ukatili wa kingono.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na shirika la jukwaa la utu wa mtoto (CDF) unasema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano matukio ya ukatili wa kingono, ubakaji na ulawiti dhidi ya watoto yamekukwa yakiongezeka na Hilo limedhihirishwa na mkurugenzi wa upelelezi makosa ya jinai (DCI) Camilius Wambura mnano tarehe 12 julai alipongea na waandishi wa habari mkoani Dodoma.
“Mikoa inayoongoza kwa ukatili kwa watoto ikiwemo mauaji, kubaka na kulawiti ni Arusha ambapo idadi ya matukio ni 1,69, Ilala 1,486, Tanga 1,347, Kinondoni 929 na Lindi 780,” ilieleza taarifa hiyo.
Aidha kwa taarifa ya mwaka 2020 ya takwimu za jeshi la polisi kupitia Dawati la jinsi na watoto imeonyesha kuwepo kwa makosa 42187 ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi Tanzania ambapo watu wazima ni 26333( wanaume 11102, wanawake 1523) na watoto 15854(wakiume 3012, wakike 12842) ambapo pia taarifa hiyo inaonyesha kuwa jumla ya wanawake 1284 na watoto 5867 walibakwa ndani ya mwaka 2020 na watoto 1000(wakiume 885, wakike 115) walilawitiwa.
Kama sehemu ya kuimarisha mifumo ya ulinzi, utoaji na upatikanaji wa haki jinai kwa watoto nchini Tanzania CDF imekuwa ikishirikiana na taasisi ya Irish Rule of law International (IRLI) ya nchini Ireland kutekeleza shughuli mbalimbali zenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa haki jinai kwa watoto nchini Tanzania kwa ufadhili wa ubalozi wa Ireland Tanzania.
CDF na IRLI wameona uwepo wa uhitaji wa kufanya mkutano na makamanda na makamishana wa polisi wa mikoa kutoka bara na visiwani ili kujadili kwa pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma na upatikanaji wa haki jinai kwa watoto waliopitia ukatili wa kingono.