Home LOCAL MAMILIONI YA WATU WAISHIO VIJIJINI WANUFAIKA NA UWEKEZAJI WA SBL KWENYE MAJI...

MAMILIONI YA WATU WAISHIO VIJIJINI WANUFAIKA NA UWEKEZAJI WA SBL KWENYE MAJI SAFI NA SALAMA

 
Upatikanaji wa maji umekuwa mwiba kwa baadhi ya maeneo ya nchi, ambapo watu hupita siku kadhaa bila kuyapata huku wengine wakikabiliwa na mgao. Halikadhalika, Serikali imeshatoa hali ya tahadhari kwa watumiaji huku Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) ikiwaomba watumiaji kuhifadhi maji kila yanapotoka. Hii ni kutokana na upungufu wa kina cha maji katika maeneo ya Ruvu Juu na Mto Wami, changamoto inayosababishwa na ukosefu wa mvua.

Hata hivyo, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amewahakikishia Watanzania kuwa ofisi yake inachukua kila hatua ili kukabiliana na hali hiyo. Aidha, Waziri alisema wamekuwa wakifanya mageuzi makubwa ya kitaasisi, kifedha na kiufundi ili kupata huduma ya maji iliyo endelevu. Alisema, ‘hadi sasa kuna wakala wa usambazaji maji vijijini wapatao 2,115 unaojumuisha wahasibu 1,362 na wataalam 1,611 katika maeneo ya vijijini’.

Wakati hayo yote yakiendelea, kampuni pendwa ya bia, Serengeti Breweries Limited (SBL) iko mstari wa mbele kuwekeza katika miradi ya maji safi na salama kwa mamilioni ya wakazi wa vijijini nchini Tanzania. Miradi hii ya maji imepewa jina, Water of Life, wenye lengo la kuchochea jumuiya yenye maendeleo endelevu. Mpango huu umeanishwa kwenye mkakati wake wa maendeleo wa muda mrefu unaoitwa Society 2030; Spirit of Progress.

Tangu mwaka 2010, SBL imetumia zaidi ya TZS 1.1bn/- kuchimba visima 18 nchini kote, jambo ambalo limechangia kupunguza uhaba wa maji nchini. SBL pia imeshirikiana na mashirika mengine kwenye ujenzi wa miradi hiyo ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata maji safi na salama katika baadhi ya maeneo yenye uhitaji zaidi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya SBL, John Wanyancha alisema kuwa SBL inachukulia maji kuwa jambo muhimu sana kwenye ustawi wa jamii, na ndiyo maana inashirikiana na Serikali na wadau wengine wa maendeleo kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama nchini.

Mwaka huu SBL ilizindua mradi wa maji wenye thamani ya Tsh milioni 220 katika kijiji cha Machochwe wilaya ya Serengeti mkoani Mara kwenye jitihada zake za kupeleka maji safi na salama vijijini. Mradi huu na uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 12,000. Mradi huu pia unajumuisha kisima na mifumo yake, pampu ya maji inayotumia nguvu ya jua na tanki la maji linaloweza kutoa lita 7,500 za maji kwa saa.

Vilevile SBL imewekeza kwenye mikoa mingine ya Iringa, Kilimanjaro, Mwanza, Tanga, Ruvuma, Dar es Salaam, Pwani na Dodoma ikiwapatia wanufaika zaidi ya milioni moja maji safi na salama. “SBL imeweka sera ya makusudi kusaidia ustawi wa jamii yetu Maji ikiwa ni mojawapo la maeneo manne ya kipaumbele ambayo kampuni yetu imeainisha katika malengo yake ya kutoa msaada wa kijamii“, alisema Wanyancha. Alifafanua pia vipaumbele vingine vya kampuni kama utoaji wa stadi za maisha, utunzaji wa mazingira na elimu juu ya athari ya unywaji pombe kupita kiasi.

Zaidi ya hayo, miradhi hii ya maji pia imelenga kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa nafaka zao kama vile mahindi, mtama na shayiri ambazo ni malighafi muhimu sana katika utengenezaji wa bia. Mfano, mwaka 2020 pekee, SBL ilipata tani 17,000 za nafaka hizi ndani ya nchi, sawa na asilimia 70 ya mahitaji ya mwaka ya malighafi ya SBL kutoka kwa mtandao wa wakulima 400. Kufikia 2025, SBL imelenga kuongeza upatikanaji wa malighafi hadi asilimia 85. SBL pia inasaidia wakulima kwa kuwapa mbegu bure, kuwapa huduma za kiufundi za shambani na kuwaunganisha na taasisi za kifedha.

Ni jambo lisilopingika kwamba SBL imeweka hatua madhubuti za kusaidia maendeleo ya jamii kama kwenye uwekezaji wa maji safi na salama hususani nyakati hizi za uhitaji mkubwa wa maji nchini. Na kwa wakazi wa vijijini uwekezaji huu umeleta faraja ukizingatia ya kuwa bado kuna baadhi ya maeneo upatikanaji wa maji umekuwa mgumu sana na vyanzo vyake kutokuwa salama kwa afya zao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here