Home LOCAL DKT. GWAJIMA AWATAKA WALIMU KUSIMAMIA NIDHAMU

DKT. GWAJIMA AWATAKA WALIMU KUSIMAMIA NIDHAMU


Na: WAMJW-TABORA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa viongozi na walimu wa chuo cha St.Maximillian kusimamia nidhamu ya wanafunzi ili kupata wanafunzi bora wenye weledi na kufuata maadili ya taaluma yao.

Dkt. Gwajima ametoa wito huo leo Novemba 27, 2021, kwenye mahafali ya kwanza ya Chuo cha St.Maximillian kilichopo Mkoani Tabora.

Dkt. Gwajima amesema, Pamoja na upungufu wa wataalamu katika Sekta ya Afya nchini, ametoa wito kwa Uongozi na Walimu wa Chuo hicho kuendelea kusimamia nidhamu na maadili ya wanafunzi katika chuo hicho.

“Pamoja na upungufu wa Wataalamu katika Sekta ya afya nchini, ninawaomba msimamie sana nidhamu ya wanafunzi ili tupate wahitimu ambao ni salama katika kutoa huduma.” Amesema.

 

Aliendelea kusema kuwa, amekua akipokea malalamiko mbalimbali ya wananchi kuhusiana na huduma wanazopata kutoka kwa baadhi ya wataalamu wetu katika vituo vya kutolea huduma za afya, hali ambayo ni kinyume na maadili ya taaluma ya kada za Afya.

Aidha, Dkt. Gwajima ameupongeza uongozi wa Chuo cha St.Maximillian, na kuweka wazi kuwa, Serikali inatambua juhudi kubwa zinazofanywa na Sekta Binafsi katika kuzalisha Wataalamu wa Afya  ukizingatia kwamba kuanzisha na kuendesha mafunzo ya Kada za Afya ni gharama kubwa.

Kwa upande mwingine Dkt. Gwajima amewapongeza wahitimu kwa kufikia ngazi ya masomo ambayo itawapa fursa  ya kuajiriwa, kujiajiri au kujiunga na masomo ya vyuo vikuu.

“Naomba kutumia fursa hii kuwapongeza wahitimu kwa kufikia ngazi hii ya masomo ambayo itawawezesha kuajiriwa, kujiajiri au kujiunga na masomo ya vyuo vikuu.” Amesema.

 

Mbali na hayo amesema,  bado Dunia ipo kwenye mapambano dhidi ya UVIKO-19, tayari baadhi ya nchi za Ulaya zimeingia Wimbi la nne la Ugonjwa wa Corona, hivyo nawasisitiza tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ikiwemo kuendelea kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19. Amewataka

“Ugonjwa wa COVID-19 bado upo,  Nimefurahi kusikia kwamba mpo mstari wa mbele kwenye uhamasishaji kwa wananchi kuchanja chanjo ya UVIKO-19 ili kujikinga wao pamoja nabfamilia zao” Amesema Dkt. Gwajima.

Nae, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambae pia ni Mganga Mkuu Mkoa wa Tabora Dkt. Honoratha Rutatinisibwa amesema, Chuo cha St.Maximillian kimekuwa ni chuo muhimu katika Sekta ya Afya, kwani licha ya wanafunzi wake kwenda kujifunza katika vituo vya kutolea huduma za afya wanafunzi hao wamekuwa msaada mkubwa kuchochea ubora wa huduma kwa wananchi.

Pia, amesema kuwa,  Chuo hicho kimekuwa ni msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya UVIKO-19, kwani kimekuwa kikitoa elimu na hamasa kwa wananchi wa Tabora kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19.

Mbali na hayo, amempongeza Waziri wa Afya kwa kutenga muda na kufika katika chuo cha St.Maximillian katika mahafali ya kwanza ya Chuo cha St.Maximillian kilichopo Mkoani Tabora.

Mwisho.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here