Home BUSINESS MWENYEKITI MTENDAJI WA SHELL ATETA NA BALOZI WA TANZANIA

MWENYEKITI MTENDAJI WA SHELL ATETA NA BALOZI WA TANZANIA

Makamu wa Rais na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Shell ya Uholanzi mwenye makazi yake Tanzania, Bw. Jared Kuehl alitembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Uholanzi na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Irene Kasyanju hivi karibuni. 

Katika mazungumzo hayo, Pamoja na mambo mengine, Bw. Kuehl alimhakikishia Balozi Kasyanju utayari na dhamira ya dhati ya Kampuni yake kuendelea kuwekeza Tanzania kwa kutekeleza Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (Liquified Natural Gas – LNG) kwa kushirikiana na Kampuni ya Equinor ya Norway. 

Bw. Kuehl alisema anafurahishwa na ushirikiano ambao Ofisi yake (Shell Exploration & Production Tanzania Ltd) imekuwa inapata nchini Tanzania na kwamba hatua zinazochukuliwa na Serikali hivi sasa ni za kuridhisha wakati kampuni hiyo inapojiandaa kufanya majadiliano ya pamoja yanayolenga kufanikisha utekelezaji wa Mradi wa LNG.

“Kimsingi nKampuni ya Shell imefurahishwa na uamuzi wa Serikali kukubali Kampuni hizi mbili ziungane na zifanye kazi pamoja na namna inavyoandaa taratibu zinazohusu masuala ya kisheria na kiufundi, udhibiti wa Mradi pamoja na masuala ya kikodi yanayohusu Mradi huo wa NLG nchini”, Bw. Kuehl alisema.

Kwa upande wake, Balozi Kasyanju alifurahishwa na ujio wa Kiongozi huyo na kutumia fursa hiyo kumshukuru kwa kufika Ubalozini, kuishukuru Shell na Equinor kuwekeza Tanzania, na kuelezea matarajio yake kwamba uwekezaji huo utakuwa ni wa manufaa kwa pande zote mbili. Alimhakikishia Makamu wa Rais na Mwenyekiti Mtendaji huyo ushirikiano endelevu wa Ubalozi wake na wa Serikali nzima kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here