Na: Projestus Binamungu, WHUSN, Biharamulo
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasimu Majaliwa, kusimamia michezo katika ngazi zao ili kuwawezesha vijana kukuza vipaji vyao vya michezo kupitia sekta hiyo.
Waziri Bashungwa amewakumbusha viongozi hao kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya kikazi na viongozi wa wilaya ya Biaharamulo mkoani Kagera na wilaya ya Bukombe mkoani Geita katika ligi mbili tofauti katika wilaya hizo.
Akizungumza katika vikao na viongozi ngazi ya wilaya, Waziri Bashungwa amesema Makatibu Tawala ndio wenye jukumu la kusimamia michezo kwa ngazi ya mikoa na wilaya ambapo wamepewa mamlaka hayo kupitia Sera ya Michezo ya mwaka 1995.
“Kwa mujibu wa Sera hiyo, hawa ndiyo wenyeviti wa kamati za michezo za ngazi ya mikoa na wilaya, hivyo wanawajibika moja kwa moja kukuza vipaji vya vijana kupitia michezo” amesema Waziri Bashungwa.
Sambamba na hilo, Waziri Bashungwa ameliagiza Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa kushirikiana na Baraza la Michezo nchini (BMT) pamoja na Chuo cha Michezo cha Malya kuangalia uwezekano wa kuwawezesha walimu wa michezo kutoka katika chuo hicho kutembelea maeneo mbalimbali katika ngazi ya wilaya na vijiji kutoa elimu elekezi ya uamuzi wa mchezo wa soka nchini ili kujenga uelewa unaolenga kuleta tija kwa wachezaji na taifa kwa ujumla.
Akiwa ziarani katika mikoa ya kanda ya Ziwa, Waziri Bashungwa ameshiriki kufunga mashindano ya ligi mbili za ngazi ya wilaya ambazo ni “Engineer Ezra Cup” yaliyodhaminiwa na Mbunge wa jimbo Biharamulo mkoani Kagera Mhandisi Ezra Chiwelesa pamoja na mashindano ya “Doto Cup” yaliyodhaminiwa na Waziri wa Madini na Mbunge wa jimbo la Bukombe Mhe. Doto Biteko.