Na: Mwandishi Wetu.
WADAU wa maendeleo katika Jimbo la Ubungo na Kata ya Makurumla mkoani Dar es Salaam wamejitokeza kwa wingi kwenye mbizo za mwendo wa pole( Jogging)zilizoandaliwa kwa lengo la kuchangisha fedha kufanikisha ujenzi wa matundu ya vyoo kwa Shule za Msingi ndani ya Kata hiyo.
Jogging hiyo imeandaliwa. na Diwani wa Kata hiyo Bakari Kimwanga ikiwa ni mkakati wake wa kuchangisha fedha kwa ajili ya kujenga matundu 170 ya vyoo kwa shule hizo na kupitia mbio hizo wamefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh.milioni 20.
Katika mbio hizo zaidi ya washiriki 1,500 wamejitokeza kuunga mkono jitihada za Kata ya Makurumla na mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo katika Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akihitimisha mbio hizo za kilometa 10 zilizoanza saa 12 asubuhi hadi saa tatu asubuhi ,Profesa Kitila amempongeza Diwani wa Makurumla kwa kuandaa jogging kwa ajili ya kuchangisha fedha zitakazokwenda kutumika kujenga matundu ya vyoo kwa shule za msingi ndani ya Kata hiyo.
“Wananchi wa Kata ya Makurumla naomba niwawaambi ukweli,mmpeta Diwani mjanja sana,mmepata diwani anayejua wajibu wake katika kushirikiana na wana Makurumla na jimbo la Ubungo kuleta maendeleo.Hata mimi amekuwa akinisaidia sana kunisemea yale ambayo wananchi wanatakiwa kuyasikia.
”Yapo baadhi ya majimbo yamekosa ushirikiano baina ya madiwani na Mbunge, lakini katika jimbo langu la Ubungo ninayo bahati,nimepata madiwani ambao tunashirikiana kwa karibu kutatua changamoto za wananchi, Diwani wa kata ya Makurumla ni kielelezo tosha cha haya ninayosema, nami naahidi kuchangia Sh.500,00 kwa ajili ya kuanza safari ya kufanikisha ndoto ya diwani wetu,lazima tumuunge mkono,”amesema Profesa Mkumbo.
Pia amewapongeza wananchi na wadau wote ambao wamejitokeza kushiriki mbio hizo na kubwa zaidi namna ambavyo wameamua kwa vitendo kuwa sehemu ya kufanikisha mipango ya kujengwa kwa matundu hayo ya vyoo kwa shule za msingi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Makurumla Bakar Kimwaga amesema lengo la kuandaa mbizo hizo mbali ya kuuimarisha afya ,ni kuhakikisha wanachangisha fedha ili kujenga matundu ya vyoo kwa shule za msingi.
”Shule zetu za msingi matundu ya vyoo yapo lakini utafiti ambao nimeufanya yaliyopo hayatoshelezi, hivyo tumeamua kuandaa jogging ili kuwaleta waadau pamoja na kisha kuchangishana fedha, tunashukuru tumeanza vizuri,leo peke yake zimepatikana zaidi ya Sh.milioni 20,”amesema Kimwanga.
Amefafanua kwamba ndani ya kata ya Makurumla kuna vikundi vingi vya Jogging,hivyo aliona iko haja ya kuwashirikisha kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo kufanikisha jambo hilo.”Tunashukuru Mungu tumeanza vema, tutafanikiwa katika hili ,tunampongeza mbunge wetu Profesa Mkumbo kwa kutuunga mkono kwani huu ndio mwanzo,”amesema Kimwanga.