Home LOCAL SERIKALI KUTUMIA RASILIMALI ZA NCHI KUINUA UCHUMI WA WATANZANIA

SERIKALI KUTUMIA RASILIMALI ZA NCHI KUINUA UCHUMI WA WATANZANIA

 

  Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Maonesho ya Nne ya Tekinolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yaliyofanyika eneo la Bombambili mjini Geita, Septemba 22, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinachangia katika kuinua uchumi wa Watanzania.  

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, anawaahidi kuendelea kuchukua hatua madhubuti katika kulinda na kuendeleza rasilimali hizi ili ziweze kuwanufaisha na kuwaletea maendeleo Watanzania wote, tuendelee kuunga mkono.”

Waziri Mkuu ameseyasema hayo leo (Jumatano, Septemba 22, 2021) baada ya kuzindua Maonesho ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini mkoani Geita. Amesema maonesho hayo yamekuwa na manufaa makubwa katika kuhamasisha wananchi kujihusisha na shughuli za madini.

Amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kufanya marekebisho ya baadhi ya kanuni na taratibu zinazosimamia uchimbaji na biashara ya madini kwa lengo la kuwezesha wananchi na wadau mbalimbali kushiriki ipasavyo katika uchumi wa madini na kuongeza uwekezaji.

Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wadau wa sekta ya madini nchini wazingatie na wafuate sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia sekta hiyo ili kuondoa usumbufu na kurahisisha utendaji wa shughuli zao na Serikali kwa manufaa ya pande zote. 

Amesema sekta ya madini imeendelea kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa na maendeleo ya mtu mmoja mmoja nchini. “Matarajio ya Serikali ni kuongeza zaidi mchango huo kupitia shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, usafishaji madini, usanifu madini na utoaji wa huduma katika shuguli za madini.”

“Lengo la Serikali ni kufungamanisha ustawi wa sekta ya madini kwa kuwezesha wananchi na wadau mbalimbali kushiriki ipasavyo katika uchumi wa madini na kuongeza uwekezaji ili kukuza sekta nyingine za kiuchumi na huduma zikiwemo viwanda, ujenzi, usafirishaji, mawasiliano na nishati.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuimarisha Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili ziweze kutoa huduma bora na nafuu kwa wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na uchorongaji wa miamba ili kujua uwepo na wingi wa mashapo.

Amesema hatua hiyo, itasaidia wachimbaji wadogo kuendesha shughuli zao kwa tija na uhakika na hivyo, kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi. “Natoa wito kwa wachimbaji kutumia taasisi hizi ili muweze kupata taarifa za mashapo ya madini na kuchimba kwa uhakika.”

“Katika hili, ninaielekeza Wizara ya Madini ihakikishe suala la Local Content (kipengele cha ushirikishwaji wa wazawa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati) linasimamiwa kikamilifu. Aidha, makampuni yote makubwa yatumie huduma za GST na STAMICO ispokuwa pale ambapo itathibitika wameshindwa ndipo waagize nje.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya madini nchini ili kuiwezesha kufikia lengo la kuchangia asilimia 10 ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2025. “Ni ukweli usiopingika kwamba suala hili litafanikiwa endapo wadau wote tutashirikiana kuanzia hatua ya utafutaji, hadi biashara ya madini.”

Ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa vijana, wanawake na Watanzania wote kwa ujumla wachangamkie fursa zilizopo na zitakazojitokeza kwenye maeneo mbalimbali ya miradi ya madini nichini ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

“Nyote mtakubaliana nami kuwa kuna miradi mingine mikubwa inatazamiwa kuanza hivi karibuni ukiwemo mradi wa Nyanzaga Mining uliopo Wilaya jirani ya Sengerema na mgodi wa madini ya Rare Earth Element uliopo Songwe. Kwa hiyo, jipangeni vizuri na mchangamkie fursa hizo.” 

Amesema Serikali katika mwaka 2021/2022 imefuta tozo ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa madini kutoka nje ya nchi yatakayouzwa kwenye masoko au kusafishwa nchini kwa lengo la kuimarisha biashara baina ya nchi yetu na nchi nyingine. Hatua hizi, zinalenga kuboresha mazingira ya biashara ya madini nchini.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kote  duniani waje kwa wingi kusafisha, kuuza na kununua madini kwenye masoko yetu yaliyotapakaa nchi nzima. “Najua hata ninyi wachimbaji wetu hapa baadhi yenu mna migodi nchi jirani basi leteni madini yenu hapa muuze kwa uwazi na uhakika kwenye masoko yetu.”

Kwa upange wake, Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko amesema Wizara ya Madini itaendelea kusimamia biashara ya madini nchini ili kuhakikisha ndoto ya Rais Mheshimiwa Samia ya kutaka kuona Tanzania inakuwa kitovu kikubwa cha biashara ya madini inatimia.

Naye,  Rais wa Muungano wa Wachimbaji Wadogo  Tanzania,  John Mbina ameipongeza Serikali kwa namna inavyosimamia ukuaji wa sekta ya madini nchini. “Wachimbaji wadogo wameendelea kuleta mapinduzi ya kikodi, mwaka jana walichangia shilingi bilioni 180, hii ni ishara kwamba siku moja wachimbaji wadogo watasogea na kuwa wachimbaji wakubwa”

Awali, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR) kinachimilikiwa na Mtanzania kilichopo eneo la Bombambili ambapo amesema kuwa Serikali itafanya jitihada ili kuhakikisha kiwanda hicho kinafanya kazi kama ilivyokusudiwa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa GGR, Sarah Masasi kuiomba Serikali isaidie ili kiwanda hicho kinachotumia teknolojia ya kisasa kiweze kufanya kazi. Gharama ya ujenzi na ununuzi wa mitambo ya kiwanda hicho ni shilingi bilioni 28.

Naye, Ofisa Mtendaji Mkuu wa GGR, Sarah ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali pamoja na Wizara ya Madini kwa ushirikiano inaompatia katika kuhakikisha uwekezaji huo unafanyika. Amesema kiwanda hicho kitasafisha dhahabu kwa kiwango cha kimataifa na itauzwa katika masoko mbalimbali duniani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here