Home LOCAL RC MKIRIKITI: TMDA ELIMISHENI VIONGOZI WA VIJIJI KUDHIBITI MADAWA NA VIFAA TIBA...

RC MKIRIKITI: TMDA ELIMISHENI VIONGOZI WA VIJIJI KUDHIBITI MADAWA NA VIFAA TIBA MIPAKANI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akiwa ameshika machapisho ya taarifa za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba kuhusu udhibiti wa uingizwaji holela wa dawa na vifaa tiba leo ofisini kwake Sumbawanga. Kushoto ni Anitha Mshighati Kaimu Meneja wa TMDA Nyanda za Juu Kusini.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akiwa kwenye mazungumzo na wataalam wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba toka Mbeya waliopo mkoani Rukwa kwa ukaguzi ambapo amewataka watoe elimu kwa viongozi waliopo mipakani ili wadhibiti uingizwaji wa dawa na vifaa tiba visivyo na ubora.
 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akizungumza na wataalam wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba waliofika ofisini kwake Sumbawanga leo.
 
Na: Amani Kassimba, RUKWA.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeshauriwa kuelimisha na kuwatumia viongozi wa vijiji na tarafa hususan waliopo mipakani kudhibiti uingizwaji wa vifaa tiba na madawa yasiyo na ubora toka nje ya nchi visisambae mkoani Rukwa.

Kauli hiyo imetolewa  na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti wakati alipokutana ofisini kwake na wataalam wa TMDA Nyanda za Juu Kusini toka Mbeya leo (15.09.2021) mjini Sumbawanga ambao wapo mkoani Rukwa kwa kazi ya ukaguzi wa madawa na vifaa tiba kwenye halmashauri .

“Tumieni uwepo wa mifumo ya kiutendaji ya serikali iliyopo kuanzia vijiji na tarafa hususan kwenye mipaka yetu na nchi za jirani ambako kwa uchunguzi wenu ndiko vifaa tiba na madawa mengi yasiyo na ubora hupitia kuingia nchini ikiwemo kwenye mkoa wa Rukwa” alisema Mkirikiti.

Mkirikiti amewakaribisha wataalam hao kuandaa taarifa ya hali ya uingiaji vifaa tiba na madawa yasiyo na ubora ikiwemo mikakati yao ya kudhibiti ili kuikinga jamii na matumizi yasiyo sahihi ya bidhaa hizo ambapo wataweza kuwasilisha kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) mwezi ujao.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Nyanda za Juu Kusini Anitha Mshighati alisema tatizo la uingizwaji vifaa tiba na madawa yasiyokidhi viwango ni kubwa kwenye maeneo ya mpakani na nchi za Congo na Burundi .

Aliongeza kusema jitihada za mamlaka ni kuendelea kuzishi Mamlaka za serikali za mitaa mkoani Rukwa kushirikiana na TMDA ili kudhibiti uingizwaji wa madawa kinyume cha taratibu za nchi.

“Katika ukaguzi wetu wa mwezi Agosti mwaka huu tumebaini bado changamoto ya dawa na vifaa tiba kuingizwa nchini kinyemela kwenye mipaka ya mkoa wa Rukwa na nchi za jirani husuan Ziwa Tanganyika. Tunaomba mkoa usaidie udhibiti wake kwa kutumia vyombo vya dola” alisema Anitha.

Katika hatua nyingine Anitha  alimhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kuwa wataalam wa TMDA wataendelea kushirikiana na Viongozi wa chama na Serikali katika kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba vyenye kuzingatia ubora na vilivyothibitishwa na TMDA ili kulinda afya za watanzania na uchumi wa nchi.

Mwisho. Imeandaliwa na ;

Afisa Habari Mkuu,

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa,

SUMBAWANGA

15.09.2021

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here