Na: Beatrice Sanga, MAELEZO, Dar.
Septemba 06, 2021.
WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka Taasisi za Serikali zinazotoa huduma kwa wananchi, ambazo hazijajiunga na utaratibu wa Vituo Huduma pamoja vilivyopo kwenye Shirika la Posta Tanzania, kujiunga na huduma hiyo ndani ya mwaka huu wa 2021-2022 ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Amesema ilani ya chama cha Mapinduzi ya 2020 inaelekeza serikali kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali kwa umma, kwa kuanzisha vituo vya huduma ya pamoja ili kuongeza ufanisi ambapo mradi wa huduma hiyo iliyopo Posta ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kitaifa wa ‘Tanzania ya kidijitali’ na kuzitaja Taasisi na Wizara ambazo zinatakiwa kujiunga na huduma hiyo kuwa ni pamoja na Wizara ya Ardhi, Wizara ya Utumishi (Tume ya Ajira), TIC, TMDA, NEMC, EPZA na TBS.
Ameyasema hayo Septemba 06 2021 alipokuwa akizindua rasmi mradi wa vituo vya Huduma Pamoja wa Shirika la Posta Tanzania, Hafla iliyofanyika katika viwanja vya makao makuu ya shirika hilo Jijini Dar es Salaam ambapo vituo vya huduma pamoja vilivyozinduliwa ni Idara ya Uhamiaji , Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhaminia (RITA), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
“Nazielekeza taasisi zote zinazotoa huduma kuongeza kasi ya kujiunga na utaratibu wa huduma pamoja taasisi ambazo hazijaanza kutoa huduma sasa zijipange kuhakikisha kuwa zinatoa huduma katika vituo hivi ndani ya mwaka huu 2021- 2022” Amesema Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk. Faustine Ndungulile ameishukuru serikali ya awamu ya sita ambayo ilianza kuja na mradi wa vituo vya huduma pamoja, ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma kwa urahisi na haraka.
Dkt. Ndugulile amesema vituo hivi vina lengo la kuweka pamoja watoa huduma na wateja wao, ili kurahisisha huduma za serikali ambapo mpaka sasa, serikali imetoa fedha za awali Sh Bilioni 3.9 na fedha hizo zitaelekezwa katika dijitali posta (digital postal) pamoja na kununua nyenzo zitakazorahisisha usafirishaji kupitia posta na kuahidi kufanya mabadiriko makubwa ndani ya shirika lengo likiwa ni kuifanya posta, kuwa posta ya kidijitali.
“sisi kama wizara tumezamiria kwamba tunafanya mabadiliko makubwa sana ndani ya shirika letu la posta na mimi kama Waziri nina ridhika na hatua za awali na mafanikio ambayo yamefikiwa na shirika letu la posta. tumedhamiria kuhakikisha kwamba posta yetu inakwenda kuwa posta ya kidigitali” Amesema Dkt. Ndungulile.
Naye Kaimu Posta Masta Mkuu Bw. Macrice Mbodo, ameeleza kuwa, utekelezaji wa mradi wa huduma ya pamoja utatekelezwa kwa awamu tatu, ambapo awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa kipindi cha miezi 18 kilichoanza Mwezi Julai 2021 mpaka Desemba 2022 ampapo katika awamu hii, huduma za serikali zitatolewa kwa wananchi katika mtindo wa huduma moja dirisha moja(multiple window system), na kila dirisha litakuwa linahudumia mwananchi katika dirisha lake, ambapo vituo kumi , vinatarajiwa kufunguliwa vikiwemo vituo vya Dodoma, Arusha, Mbeya, Mwanza, Tanga Kigoma, Unguja na Pemba. Ameendelea kueleza kuwa, katika awamu ya pili vituo kumi na saba vinatarajiwa kufunguliwa ambavyo vitahusisha vituo vya Pwani Iringa Rukwa Ruvuma, Kilimanjaro, Tabora, Mara, Lindi, Mtwara, Manyara, Katavi, Njombe na Geita.
Aidha,kipindi cha awamu ya tatu ya mradi huu utahusisha kipindi cha miezi 18 Julai-Disemba (Single Window System) itakayoanza Julia 2024 dec 2025 katika awamu hii huduma za serikali zitaanza kutolewa katika mtindo wa dirisha moja huduma zote ( single window system )ambapo vituo vitafunguliwa katika Wilaya zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwisho.