Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ameliagiza Baraza la Uuguzi na Ukunga kuwachukulia hatua Wauguzi na Wakunga wote wanaovunja Sheria, maadili, miongozo na miiko ya taaluma Yao bila kuwaonea.
Dkt. Gwajima ametoa agizo hilo mapema leo Septemba 18, 2021 wakati akizindua Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, tukio lililofanyika katika Ukumbi wa kituo hicho kilichopo Kibaha, Mkoani Pwani.
Amesema, Baraza lina wajibu mkubwa wa kuhakikisha linalinda, kuimarisha na kuhifadhi Afya ya Jamii, Usalama na Ustawi kupitia usimamizi na udhibiti wa shughuli za mafunzo ya Uuguzi na Ukunga, huku akiweka wazi kuwa karibu asilimia 60% ya Watoa huduma za afya hapa nchini ni Wauguzi na Wakunga ukilinganisha na kada nyingine.
Aliendelea kusema kuwa, Bado taaluma hii inazo changamoto hasa katika upande wa utoaji huduma kwa wananchi, hali inayopelekea kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, hivyo kuliagiza Baraza hilo kusimamia vizuri utoaji huduma bora na salama kwa wananchi.
“Bado tunazo changamoto katika taaluma hii, hususani katika utoaji wa huduma ambako tunaendelea kupokea malalamiko mengi hutoka kwa jamii. Hivyo, Baraza hili linatakiwa kuhakikisha kuwa jamii yetu inapata huduma bora na salama.” Amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Bi. Ziada Sellah amempongeza Mhe. Waziri wa Afya kwa uteuzi makini wa Baraza la Uuguzi na Ukunga ambalo litakuwa chachu ya kuleta matokeo chanya kwenye usimamizi na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kufuata Sheria na Kanuni za Uuguzi na Ukunga nchini.
Hata hivyo, ametoa rai kwa Baraza jipya kushughulika na changamoto za Baraza hilo ikiwemo rasilimali fedha ili kuwasaidia kutekeleza majukumu ya Baraza hilo kwa ufanisi na weledi.
Mwisho.