Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo za wizzara hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amewataka wakurugenzi wa majiji, Manispaa,Miji na wilaya kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi kupitia kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ndani ya siku tano kuanzia kesho tarehe 03 Agost,2021.
Ametoa tamko hilo leo Jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari ambapo amesema wakurugenzi wawili ambao majina yao yameonekana kutokea kwenye maeneo zaidi ya moja wataripoti kwenye kituo ambacho jina limeonekana kwa mara ya kwanza kwenye orodha ya Uteuzi.
“Pale palipojirudia jina patatambulika kama nafasi wazi na itajazwa hapo baadae.Nafasi hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi na Halmashauri ya mji wa Njombe”. Amesema Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy amesema wakurugenzi ambao uteuzi wao umesitishwa wakaripoti kwa makatibu Tawala wa Mikoa mara moja na Makatibu Tawala wa Mkoa wawapokee na kuwapangia majukumu.
Pamoja na hayo Waziri Ummy amesema TAMISEMI inaandaa kikao kazi kwa ajili ya wakurugenzi wote kitakachofanyika mwezi huu Agosti, 2021 ili kuweza kuapa maelekezo kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.
Tarehe 01 Agosti,2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu alifanya uteuzi w Wakurugenzi hao ambapo wakurugenzi 45 wameendelea kuwepo kwenye vituo vyao vya kazi. wakurugenzi 70 wamehamishwa vituo vya kazi na wakurugenzi 69 ni wapya.