Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akikagua kazi za wajasiriamali wabunifu katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Buhare, Musoma alipofanya ziara chuoni hapo.
Na: Mwandishi Wetu Musoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amevitaka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kote nchini kutumia taaluma inayotolewa vyuoni hapo kuelimisha wananchi kuhusu mipango mbalimbali ya Maendeleo.
Dkt. Gwajima ametoa wito huo katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare ikiwa ni sehemu ya ziara yake Mkoani Mara.
Amesema kuwa pamoja na jitihada na kazi nzuri inayofanyika chuoni hapo, bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha Jamii inapata uelewa wa kutosha kuhusu mambo mbalimbali yanayowakabili.
“Endapo tutawekeza ipasavyo katika fani hizi za Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii, tutaepukana na magonjwa yanayotukabili kwa zaidi ya asilimia 50.” alisema Waziri Dkt. Gwajima.
Aidha amekipongeza Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare kwa kazi nzuri ya ubunifu wanayoifanya kwa kuwaandaa wahitimu na kuwajengea mazingira wezeshi kuwa wabunifu ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine.
Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa Serikali imetenga fedha nyingi kupitia mikopo ya Halmashauri kwa utaratibu wa asilimia 10 maalum kwa wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu lakini fedha hizo zimebaki bila kuombwa kutokana na walengwa kukosa elimu.
“Kwanini fedha zinabaki? Ukiritimba inawezekana unakwamisha shughuli na mipango ya Maendeleo mtoe elimu Maafisa Maendeleo ya Jamii ndio kazi yenu” alisisitiza.
Akiwa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, Waziri Gwajima alikagua shughuli mbalimbali za ubunifu zinazofanywa na wajasiriamali waliopewa elimu Chuoni hapo.
Pia Waziri Gwajima ametumia fursa hiyo kutoa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo kwa watu wote kuanzia miaka 18 na kuendelea huku akiwataka kuondokana na kauli za upotoshaji zinazofanywa na baadhi ya watu kuhusu chanjo ya UVIKO 19.
Awali, akimkaribisha Waziri Dkt Gwajima, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, Paschal Mahinyila amesema Chuo hicho kinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na uhaba wa watumishi na uchakavu wa miundombinu.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha Chuo kinatoa wataalam wa Maendeleo ya Jamii walio na tija Chuo kinatekeleza Programu za Uanagenzi inayosaidia wanafunzi kupata uzoefu.