Home BUSINESS WAZIRI WA KILIMO AENDELEA NA MKAKATI WAKE WA KUDHIBITI BEI YA MBOLEA...

WAZIRI WA KILIMO AENDELEA NA MKAKATI WAKE WA KUDHIBITI BEI YA MBOLEA NCHINI.

Na Mathias Kanali, Wizara ya Kilimo-Dar es Salaam.

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda amewasili nchini akitokea nchini Morocco ambapo pamoja na mambo mengine katika ziara yake hiyo aliitembelea kampuni ya uuzaji wa mbolea ya OCP ili kuendelea na mkakati wa serikali katika kuhakikisha kuwa mbolea inapatikana kwa wingi nchini.

Akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 20 Julai 2021 Waziri Mkenda amesisitiza kuwa Serikali inaendelea na mkakati wa kuhakikisha inadhibiti ongezeko la bei ya mbolea.


Amesema kuwa bei ya mbolea kwenye soko la Dunia imepanda kwa kiasi kikubwa hivyo serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa bei ya mbolea nchini inaendelea kuwa katika ustahimilivu wa bei huku juhudi zikiendelea za kuhakikisha bei ya mbolea inashuka bei.


Amesema kuwa uingizaji wa mbolea umeongezeka kwa kiasi kikubwa hapa nchini. “Hivyo natoa rai kwa wafanyabiashara wa mbolea nchini wanaohifadhi mbolea wakidhani bei itapanda, hilo hapana itashuka hivyo ni bora kuiuza mbolea hiyo mapema” Amekaririwa Waziri Mkenda


Waziri Mkenda amesema kuwa serikali haina kodi kwenye mbolea ila sehemu pekee ya gharama ilikuwa ni ucheleweshaji wa kushusha mbolea pamoja na bei ya soko la Dunia. “Sijasema kwamba bei ya mbolea itashuka sana maana bei imepanda Duniani” Amekaririwa Waziri Mkenda


Waziri Prof. Mkenda ameongeza kuwa Wizara yake tayari imefanya mazungumzo na Uongozi wa Bandari ya Dar es salaam ili kuhakikisha kuwa mbolea inapowasili bandarini inapewa kipaumbele ili iweze kupakuliwa kwa haraka na kuwafikia wakulima kwa wakati, “Kwa hili naomba niipongeze Bandari ya Dar es salaam mmeendelea kusimamia kwa ufasaha swala la upakuaji wa mbolea kwenye meli zinazowasili” Amesema.


Ameongeza kuwa ili kuhakikisha changamoto za wafanyabiashara zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka tayari Serikali imeshatoa maelekezo ya Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) kuanza kutoa vibali vya kuuza mbolea ambayo imeshaingia nchini (Export Permit) badala ya vibali hivyo kutolewa ofisi ya Waziri wa Kilimo kama ilivyokuwa awali.


Ameongeza kuwa ili kuongeza ufanisi zaidi wa utendaji vibali hivyo vitatolewa kwa njia ya mtandao (Online) badala yake Ofisi ya Waziri wa Kilimo itakuwa na jukumu la kupewa taarifa ya utekelezaji wa utoaji vibali uliofanywa na TFRA.


MWISHO

Previous articleWAZIRI LUKUVI AWASWEKA NDANI WATANO KWA UTAPELI WA VIWANJA BAGAMOYO
Next articleWAZIRI MKUU MAJALIWA KUFUNGUA MAONESHO YA TEKNOLOJIA YA MADINI SHINYANGA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here