Picha na: JKCI
Na: Mwandishi Maalum – Dar es Salaam.
Wahudumu wa afya nchini wametakiwa kuwa wakarimu wakati wanapowahudumia wateja na wagonjwa kwani kufanya hivyo wataongeza idadi ya watumiaji wa huduma watakaokwenda kutibiwa katika vituo vyao na kuvutiwa wajiunge na bima za afya na hivyo kuongeza mapato ya vituo husika na kupitia kuvutia wateja wa kimataifa watainua uchumi wa nchi kwa ujumla wake.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima wakati akizindua timu ya kuratibu hatua za Tanzania kuelekea kwenye utalii wa tiba katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Waziri Dkt. Gwajima alisema asili ya binadamu yeyote yule anahitaji kujaliwa, kuthaminiwa na kutambuliwa kama wahudumu hao wa afya wakifanya hivyo watapiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa.
“Hospitali zetu zina majengo mazuri, zina wataalamu wa kutosha na vifaa tiba vya kisasa vya kutosha kitu kinachokosekana ni ukarimu kwa wagonjwa, ili tuingie katika utalii wa matibabu kwa kila hospitali tunatakiwa kuwe na mabadiliko katika utendaji wa kazi ili mgonjwa achaguwe kwenda kutibiwa katika Hospitali yako”,.
“Imefika wakati sasa kwa hospitali kufungua kitabu cha utoaji huduma kwa mteja ili kila mfanyakazi anayelalamikiwa kwa kutoa huduma mbaya na anayesifiwa kwa kutoa huduma nzuri jina lake liandikwe humo, yule atakayelalamikiwa mara nyingi aweze kuchukuliwa hatua na yule ambaye jina lake litaongoza kwa kutoa huduma nzuri apongezwe”, alisema Dkt. Gwajima.
Waziri huyo wa Afya alisema utalii tiba siyo ngeni hapa nchini na tayari umeanza kufanyika, katika utalii huu mgonjwa anachagua hospitali ambayo inatoa huduma bora na nzuri na kwenda kutibiwa huko. Utalii huu unafanyika kwa watanzania wenyewe na kwa wagonjwa wanaotoka nje ya nchi na kuja kutibiwa hapa nchini kwa kufanya hivyo nchi inaongeza mapato pia tunaimarisha undugu kati ya nchi na nchi.
Dkt. Gwajima pia aliipongeza timu hiyo ya kuratibu hatua za Tanzania kuelekea katika utalii wa tiba na kusema inawataalamu wa kada mbalimbali wakiwemo kutoka sekta binafsi na kuwaagiza katika utekelezaji wa utalii tiba wasiziache Hospitali binafsi kwani nazo zina majengo mazuri, wataalamu wa kutosha na vifaa vya kisasa jambo la muhimu ni kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya utalii tiba kama zilivyo nchi zingine Duniani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo Prof. Mohamed Janabi alisema kamati hiyo imependekeza utalii huo uanze kufanyika katika tiba ya moyo inatolewa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), matibabu ya figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), tiba ya upasuaji wa ubongo inayotolewa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na matibabu ya mionzi ya saratani yanayotolewa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road na baadaye ufanyike katika hospitali za kanda, mikoa na wilaya.
Prof. Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI alisema katika utalii tiba kuna watalii wa aina tatu ambapo kuna wagonjwa wanakuja kutibiwa nchini kutoka nje ya nchi na baada ya kupona wanarudi nchini kwao, kuna wagonjwa watakuja kutibiwa na baada ya kupona watakwenda kutalii katika vivutio mbalimbali vya utalii na kuna watalii ambao wanakuja kutalii nchini ambao wakipata matatizo ya kiafya watapata huduma za matibabu hapa nchini.
“Jambo la muhimu ni kuangalia ni jinsi gani Hospitali zetu zitatoa huduma ambazo zitawavutia watanzania pamoja na nchi mbalimbali za Afrika kutibiwa hapa nchini na siyo kwenda kutibiwa mahali pengine kwani tuna wataalamu wa kutosha, vifaa tiba vya kisasa na majengo mazuri”, alisema Prof. Janabi.
Naye Abdulmalik Mollel ambaye ni mjumbe wa timu hiyo na mwanzilishi na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya utalii tiba ya GEL alisema hapa nchini kuna huduma nzuri za matibabu lakini kitu kinachokosekana ni lugha zinazotolewa kwa wagonjwa na wahudumu wa afya pamoja na namna ya utoaji wa huduma husika.
Alitoa mfano wa raia wengi wa visiwa vya Comoro wanavyotegemea kupata huduma za matibabu hapa nchini lakini changamoto kubwa wanayokutana nayo ni lugha wao wanazungumza lugha ya Kifaransa na Tanzania lugha zinazotumika ni za Kiswahili na Kiingereza.
“Umbali kutoka uwanja wa ndege hadi zilipo Hospitali zetu za Taifa ambazo ni Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Taasisi ya Saratani Ocean Road ni kilomita kama 10, Hospitali tatu kati ya hizi zipo katika eneo moja mahali ambapo mtu anatembea kwa miguu kutoka hospitali moja hadi nyingine”,.
“Mahali ilipo Taasisi ya Saratani Ocean Road siyo mbali na zilipo hospitali hizi zingine, hii ni tofauti na nchi zingine ambako umbali wa kutoka uwanja wa ndege hadi hospitali ni mrefu pia ilipo hospitali moja na nyingine ni mbali. Tatizo lililopo hapa kwetu ninamfahamu nani ili niende kupata huduma nzuri za matibabu lakini kama tutaamua kubadilika utalii wa matibabu unawezekana kabisa kufanyika”, .
Katikati ya mwezi wa sita mwaka huu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizindua mtambo wa Cathlab uliopo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alisema ni wakati sasa umefika kwa Tanzania kuwa nchi ya utalii tiba kwani vifaa tiba vya kisasa vipo, wataalamu wapo pamoja na hospitali nzuri zipo.
Timu ya kuratibu hatua za Tanzania kuelekea kwenye utalii tiba inawajumbe 13 kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Saratani Ocean Road, Bodi ya Utalii na sekta binafsi.