Home LOCAL TCU YAFUNGUA DIRISHA LA UDAHILI KWA MWAKA WA MASOMO 2021/2022

TCU YAFUNGUA DIRISHA LA UDAHILI KWA MWAKA WA MASOMO 2021/2022

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania Profesa Charles Kihampa akizungumza na Waandishi wa Habari (hawamo Pichani) wakati wa Mkutano wake na Waandishi hao akitangaza kufunguliwa rasmi kwa Dirisha la udahili kwa waombaji wa Shahada ya kwanza katika Taasisi za elimu ya Juu kwa Mwaka wa masomo 2021/2022.

 

Mwanasheria wa TCU Roseline Ruta (kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa Tume hiyo Yusufu Rauna (kulia) kwenye mkutano huo.

Mkurugenzi wa Idara ya Ithibati kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Dkt. Kassile Telemu (kushoto) na Afisa Ithibati wa Tume hiyo Alexander Kamwela (kulia) wakiwa kwenye Mkutano huo uliofanyika kwenye Ofisi za Tume hiyo Jijini Dar es Salaam. (PICHA NA: HUGHES DUGILO)

Na: Hughes Dugilo, Dar es Salaam.

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania imetangaza kufunguliwa kwa Dirisha la udahili kwa waombaji wa Shahada ya Kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu kwa Mwaka wa Masomo 2021/2022.


Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Prof Charles Kihampa amesema kuwa Dirisha hilo limefunguliwa rasmi leo Julai 12,2021 kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha Sita hivi karibuni nakwamba inatoa fursa kwa wanafunzi hao kuanza mapema mchakato wa kufanya Maombi kwenye vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu.


Aidha amesema kuwa Maombi yote ya udahili wa kujiunga na Shahada ya kwanza utahusu Makundi matatu ambayo ni wenye sifa stahiki za kidato cha Sita, wenye sifa stahiki za Shahada (Ordinary Diploma), na wenye sifa stahiki za Cheti cha Awali (Foundation Certificate) ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.


“Maombi yatumwe moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo muombaji amevichagua na kuchagua programu za masomo anazozipenda. Mwongozo wa programu zilizoidhinishwa kudahili na vigezo stahiki” Amesema Prof. Kihampa huku akisisiza kuwa maelezo mahususi ya jinsi ya kutuma Maombi yatatolewa na vyuo husika.


Aidha Profesa Kihampa amewataka wanafunzi wanaofanya udahili kujihepusha na watu wanaojifanya kuwa ni mawakala na kujaza fomu za makaratasi na kuwasisitiza kutuma Maombi moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielektroniki iliyowekwa na vyuo husika.


“Waombaji wote wanatakiwa kuwasiliana na Vyuo husika na kupata taarifa za kina kuhusu programu za masomo ili kijiridhisha kabla ya kutuma maombi.”


Na kuongeza kuwa “Waombaji wenye Vyeti vilivyotolewa na Mabaraza la Mitihani nje ya nchi nilazima wawasilishe vyeti vyao Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), kwa vyeti vya Elimu ya Sekondari au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa vyeti vya Stashahada ili kupata ithibati ya ulinganifu wa Sifa zao kabla ya kutuma maombi ya udahili.” Ameongeza.


Katika hatua nyingine Profesa Kihampa ametangaza kuwepo kwa Maonesho ya Vyuo Vikuu 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam kuanzia tarehe 26 Julai hadi 31 Julai, 2021 ambapo wanafunzi na wananchi kwa ujumla watapata fursa ya kuonana ana kwa ana na Vyuo vya Elimu ya Juu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here