Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Hemed Abdullah ametembelea banda la Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na kujionea mambo mbalimbali yaliyoletwa na Shirika hilo kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii.
Makamu wa pili huyo amelitembelea banda hilo leo ikiwa ndio siku ya mwisho ya Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa yaliyokuwa yakifanyika katika viwanja vya Julias Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akitoa maelezo mbele ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar namna ambavyo makaa ya mawe yanavyotumika, Mhandisi Migodi kutoka STAMICO, Mbaraka Haruni amesema mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe yanauzwa katika viwanda vya simenti.
Amesema makaa hayo ya mawe yana sifa ya kutoa joto kubwa na kukaa muda mrefu wa masaa matatu bila kuzimika na kuongeza kuwa mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe ni rafiki wa mazingira.
“Lengo la STAMICO ni kuzalisha mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe tani 20 kwa saa, ila kwa sasa hivi tutaanza kuweka viwanda vidogo vidogo kila mikoa na kwa kuanzia tutaanzia Dar es Salaam lengo ni kila mwananchi aweze kuipata hii bidhaa ya mkaa.
“Kabla ya huu mwaka kuisha bidhaa hii ya mkaa mbadala itakuwa imeshaingia sokoni, sifa moja wapo wa mkaa wetu ni kwamba unakaa muda mrefu na unatoa joto la kutosha,” amesema
Hata hivyo amesema kuwa makaa hayo ya mawe watakayozalishwa yatauzwa kwa kilo na kilo moja haitazidi kiasi cha Sh. 1000 hivyo amewataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo.