Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (Kushoto) akizungumza kuhusu mwingiliano wa mawasiliano alipotembelea mpaka Wa Horohoro Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga na kuagiza taasisi mbili za Mawasiliano za TCRA na UCSAF kuhakikisha wanatafuta suluhisho la kudumu.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesikitishwa na tabia ya baadhi ya watendaji wa makampuni ya simu nchini kuwasainisha wananchi mikataba au makubaliano yeyote ya kutumia ardhi ya mwananchi kujenga mnara kwa lugha za kigeni
Akiwa katika ziara yake ya kukagua ujenzi, uwezo na ubora wa minara ya mawasiliano katika Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga Mhandisi Kundo alitembelea mradi wa ujenzi wa mnara wa Haloteli uliopo katika Kijiji cha Tanga B ambapo baada ya kumhoji mmiliki wa eneo hilo alisema kuwa alisaini mkataba wa makubaliano ya awali ya kufanya ujenzi katika eneo lake uliokuwa kwa lugha ya Kiingereza na kivietinamu
Mhandisi Kundo amepiga marufuku kumsainisha mwananchi mkataba kwa lugha za kigeni kwasababu yeyote anayefanya hivyo lazima kutakuwa na dhamira ovu dhidi ya mwananchi ndio maana anasainishwa mkataba kwa lugha asiyo ifahamu
Aliongeza kuwa, Serikali itasimamia haki na maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha wanasainishwa mikataba kwa lugha ya Kiswahili na kiingereza ili pande zote ziweze kunufaika kwa mwananchi kusaini kitu anachokielewa na kulipwa fedha kulingana na ukubwa wa maeneo wanayoyatoa kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano
Amesema kuwa dhamira ya Wizara hiyo ni kuondoa migogoro ndani ya Sekta ya Mawasiliano kwa watoa huduma kufuata taratibu wakati wa ujenzi wa minara ikiwa ni pamoja na kupata vibali vinavyohitajika na kusaini mikataba na Serikali za vijiji kwa ajili ya ulinzi wa minara ya mawasiliano
Aidha, Mhandisi Kundo alitoa maagizo kwa watoa huduma kufanya malipo kupitia akaunti za benki kutoka kwenye kampuni kwenda moja kwa moja kwa walioingia nao mkataba ambao ni wamiliki wa maeneo waliyojenga minara ili kampuni kujiridhisha inamlipa mhusika na sio vinginevyo
Wananchi wa Kijiji cha Tanga B kilichopo katika Kata ya Kwabada Wilayani Muheza walikiri mbele ya Naibu Waziri huyo kuwa wanahitaji mnara huo wa kampuni ya Halotel ujengwe kwa ajili ya kuwapatia mawasiliano baada ya kampuni hiyo kuhakikisha imefuata taratibu za kupata vibali vinavyohitajika
Kabla ya kufika katika Kijiji hicho Mhandisi Kundo alifanya ziara katika mpaka wa Horohoro uliopo katika Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga ambapo alikagua Kituo cha Huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na kukagua Jengo la TRA lililounganishwa na huduma za Mkongo huo pamoja na kukagua mwingiliano wa mawasiliano na nchi jirani ya Kenya ambapo iligundulika kuwa Kampuni ya simu ya Vodacom imefanikiwa kuzuia muingiliano wa mawasiliano katika mpaka huo
Ili kudhibiti mwingiliano wa mawasiliano katika maeneo ya mipaka, Mhandisi Kundo alielekeza taasisi mbili za mawasiliano ambazo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuhakikisha wanakuja na majibu ya kupaa suluhisho la kudumu tatizo la muingiliano wa mawasiliano katika maeneo yote ya mipaka nchini ifikapo tarehe 16 AQgosti,2021.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari