Wazee wa Kijiji cha Msiu na wageni wao wakiwaangalia ng’ombe hao watakaochinjwa kesho.
Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro akitoa maelezo na taratibu za ibada hiyo.
Na:Boniphace Jilili na Dotto Mwaibale, SINGIDA.
TAASISI za kiislamu zinazohusika na ibada ya kuchinja zimetakiwa kutekeleza ibada hiyo kwanza kwa walengwa badala ya kuwaweka nyuma.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida Issa Nassoro wakati wakikagua na Taasisi iliyotoa sadaka ya wanyama watakao chinjwa eneo litakalo tumika kwa ajili ya kuchinja ambalo lipo katika kijiji cha Msiu Wilayani Mkalama.
Sheikh Nassoro alisema ibada hiyo inalenga kuwasaidia watu wasiojiweza lakini mara nyingi walengwa huo huwekwa nyuma jambalo linaondoa maana halisi ya ibada hiyo.
Katika ibada hiyo inayotarajiwa kufanyika siku ya jumatano wiki hii zaidi ya ng’ombe 2,000 na Kondoo 4,000 watachinjwa ambapo wanyama hao wametolewa na Taasisi ya International Humanitarian Education of Torkey kutoka nchini Uturuki.
Aidha Sheikh Nassoro aliwashukuru wadau hao na kuwaomba pamoja na Taasisi zingine kupana wigo katika misaada wanayoitoa kwa kusaidia hata katika masuala ya Elimu,Maji na mambo mengine kwani bado jamii inahitaji misaada yao mbali na kupatiwa nyama.
Naye Mkurugenzi wa kanda ya kati kutoka Taasisi ya Education Gauge Growth Tanzania (EGG TZ) Abeid Husen al maarufu Bin Skinen alisema kuchinja ni sehemu muhimu ya ibada kwa mwiislamu hivyo walichokifanya hao waturuki ni zaidi ya Ibada.
Alisema watalisimamia zoezi hilo ili liweze kufanyika kwa utaratibu mzuri na kila mtu atakaye fika atapata nyama bila kujali itikadi wala nafasi ya mtu.
Kwa upande wake Sheikh wa Wilaya Miraji Ibrahim alishukuru ibada hiyo kufanyika kwenye wilaya yake na tayari maandalizi yanaendelea kufanyika.