Home LOCAL “SIKO SELI INACHANGIA ASILIMIA 6.7 YA VIFO VYA WATOTO WALIO NA UMRI...

“SIKO SELI INACHANGIA ASILIMIA 6.7 YA VIFO VYA WATOTO WALIO NA UMRI CHINI YA MIAKA MITANO’’- PROF. MAKUBI

 

Na: WAMJW-MWANZA.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema ugonjwa wa Siko Seli unachangia asilimia 6.7 ya vifo vyote vya watoto walio chini ya miaka mitano ikiwa ni sawa na watoto 7 kati ya 100 wanaofariki kila mwaka nchini.
Prof. Makubi amesema hayo leo  wakati wa maadhimisho ya siku ya Siko Seli duniani yenye kaulimbiu “Angaza, Tambua Ugonjwa wa Siko seli” Pamoja na uzinduzi wa mtambo wa uchunguzi wa magonjwa (MRI) na chumba cha upasuaji cha watoto katika Hospitali ya Rufaa ya kanda Bugando jijini Mwanza.
Prof. Makubi amesema Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha takribani watoto  11,000 huzaliwa na ugonjwa wa Siko seli  kila  mwaka hapa nchini, hii ni sawa na watoto 8 kati ya watoto 1000 wanaozaliwa.
‘Takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya nne duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Siko seli ikitanguliwa na nchi ya Nigeria, India na  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  Hadi sasa, Tanzania ina takribani ya wagonjwa zaidi ya 200,000 wenye Siko seli’. Amesema Prof. Makubi.
Prof. Makubi ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau imeanzisha mpango maalumu wa uchunguzi wa vinasaba vya siko seli na kuanza matibabu mapema ili kupunguza madhara yatokanayo na ugonjwa huu. 
Aidha, Prof. Makubi amesema Katika tafiti za majaribio zilizofanyika nchini, kati ya mwaka 2010 hadi 2020 zimeonesha kiwango kikubwa cha watoto huzaliwa na siko seli huku Mikoa ya kanda ya ziwa ikiongoza kuwa na watoto wengi wanaozaliwa na ugonjwa huu kuliko maeneo mengine ya nchi, ambapo kati ya watoto 100 wanaozaliwa watoto 14 waligundulika kuwa na siko seli.
Prof. Makubi pia ametaja baadhi ya mafanikio ikiwa ni pamoja na kuongezeka wagonjwa wa Siko seli wanaotibiwa katika vituo vya kutolea huduma kutoka 32,457 mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa 67,272 mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 107 pamoja na Huduma za maabara na utambuzi wa ugonjwa wa Siko seli zimeboreshwa, Mwaka 2015 ni Hospitali ya Muhimbili pekee iliyokuwa na uwezo wa kuthibitisha ugonjwa wa Siko seli kwa kutumia ‘HB Eletrophoresis’. Hadi kufikia mwaka 2021 kipimo hiki kinafanyika katika Hospitali 5 zikijumuisha Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Mbeya, Benjamini Mkapa na Hospitali ya binafsi ya-St Gemma iliyopo katika Halmashauri ya jiji la Dodoma. 
Prof. Makubi ametumia siku hiyo ya maadhimisho ya Siko Seli kukabidhi Mashine ya MRI ambayo imefungwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando ikiwa ni ya kwanza kanda ya ziwa pamoja na kuzindua chumba cha upasuaji wa watoto katika Hospitali hiyo.
MWISHO

Previous articleSERIKALI KUJENGA BARABARA ZA KISASA JIMBO LA SEGEREA
Next articleMAGANGA MKUU WA SERIKALI AFANYA ZIARA HOSPITALI YA AMANA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here