Home BUSINESS SERIKALI YAONGEZA WANYAMAPORI HIFADHI NDOGO YA LUHIRA SONGEA

SERIKALI YAONGEZA WANYAMAPORI HIFADHI NDOGO YA LUHIRA SONGEA

Baadhi ya wanyamapori ambao wameongezwa hifadhi ndogo ya asili Luhira mjini Songea na wanyamapori ambao wapo katika hifadhi hiyo iliyopo katikati ya mji wa Songea

Mhifadhi Mkuu wa Wanyamapri kutoka TAWA Asharafu Shemoka akizungumza mara baada ya kuwafikisha salama wanyamapori waliosafirishwa kutoka mkoani Arusha kwa magari hadi hifadhi ya Luhira Songea.

Mkuu wa Kikosi Dhidi ya Uajngili (KDU) Kanda ya Kusini na Msimamizi wa Hifadhi Ndogo ya Luhira Keneth Sanga akizungumza ndani ya hifadhi ya Luhira mara baada ya kukamilika  kwa kazi ya kuwaweka wanyamapori walioongezwa kutoka Arusha

Miongoni mwa wanyamapori  walioletwa katika hifadhi ndogo ya Luhira Songea

Magari ambayo yamebeba wanyamapori kutoka Arusha hadi Songea wakiwemo pofu majike mawili na dume moja na nyumbu majike wawili na dume moja.

SONGEA.

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeongeza idadi ya wanyamapori katika hifadhi ndogo ya asili ya Luhira iliyopo katikati ya Mji wa Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza baada ya kuwafikisha salama wanyama hao kwenye hifadhi ya Luhira, Mhifadhi Mkuu wa Wanyamapori wa TAWA Asharaf Shemoka amewataja wanyamapori walioletwa katika hifadhi hiyo ni nyumbu watatu kati yao dume mmoja na pofu watatu kati yao dume mmoja.

Amesema wanyamapori hao wametolewa katika  Shamba la ufugaji wanyamapori Majichai Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha na kwamba wanyama hao licha ya kusafiri umbali mrefu wamefika Songea wakiwa na hali nzuri.

Hata hivyo,amesema huo ni mpango wa awali wa kuleta wanyamapori katika hifadhi ya Luhira na kwamba wanatarajia kuongeza wanyama zaidi wakiwemo mbuzi mawe, kongoni, swalapala na wanyama wengine kadiri itakavyowezekana.

“Hifadhi ya Luhira ina eneo kubwa, ambalo linahitaji uwekezaji mkubwa,tunafikiria kuwaleta wanyama wakubwa kama twiga na simba ambao watawekwa kwenye uzio maalum(cage)’’,alisisitiza Shemoka.

Hata hivyo amesema katika awamu ya kwanza wamedhamiria kuwaleta wanyamapori 26 na kwamba wataendelea kuwaleta kadri malisho yatakavyokuwa yakiongezeka na kwamba wataanzisha bustani ndogo ndogo za wanyama ndani ya hifadhi ya Luhira.

Naye Mkuu wa Kikosi Dhidi ya Ujangili Kanda ya Kusini(KDU) ambaye pia ndiyo Msimamizi Mkuu wa Hifadhi ya Luhira Keneth Sanga amesema baada ya kuongeza idadi ya wanyamapori sasa wanatarajia pia idadi ya watalii itaongezeka.

Anatoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na mikoa ya kusini kufika katika hifadhi ya Luhira kujionea fursa za utalii zilizopo katika hifadhi hiyo  pekee ya asili nchini Tanzania iliyopo mjini Songea.

Hata hivyo amesema idadi ya wanyamapori wanaokula nyasa  kwenye hifadhi hiyo wameongezeka ambapo hivi kuna pundamilia,pofu,nyumbu,swala,ngolombwe,swalapala na wanyamapori wengine.

Hifadhi ndogo ya asili Luhira yenye ukubwa wa hekta 600  ilianzishwa mwaka 1974,ipo umbali wa kilometa saba kutoka mjini Songea.

Mhifadhi wa TAWA katika Hifadhi ya Luhira David Tesha amewataja wanyama wengine ambao wanapatikana katika hifadhi hii ni fisimaji, nyani,pongo,tumbili, kakakuona, na kobe,pia bustani hiyo ni makazi ya reptilia na ndege wa aina mbalimbali.

Tesha amesema  hifadhi ya Luhira ni eneo la asili lenye utajiri wa miti ya miyombo, misuku, mitumbitumbi, miwanga, minyonyo,mizambarau,mininga, na mikuyu,na kwamba ni miongoni mwa bustani chache zenye uoto wa asili kabisa zilizopo mjini. 

Amesema ndani ya Luhira,mtalii anaweza kufanya utalii wa kutembea kwa miguu,kupiga picha,kuangalia wanyama na ndege,utalii wa kuweka kambi(camping) na kufanya mapumziko ya mchana(picnic) hufanyika ndani ya eneo maalum.

“Watalii kutoka nje ya nchi pia wanatembelea hifadhi yetu, tumepokea watalii toka Ujerumani,Afrika ya Kusini, India, Marekani,Ufaransa,Italia, Uholanzi na wageni toka mikoa mbalimbali nchini,wanafanya utalii wa kuchunguza aina ya mimea na ndege’’,alisema Tesha.

Hifadhi ya asili ya Ruhila,inafikika kwa urahisi kwa ndege au kutumia barabara ya Njombe hadi Songea,Mtwara hadi Songea ambayo ni ya lami,ukifika Songea mjini eneo la Msamala unasafiri kwa barabara  kilometa 3.5 unatakuwa umefika bustani ya Luhira.

Malazi ya wageni yanapatikana Manispaa ya Songea ambapo wageni pia wanaweza kuweka mahema ya muda katika maeneo yaliyotengwa ndani ya hifadhi hiyo.

Imeandikwa na Albano Midelo

Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma

Juni 27,2021

           

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here