SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inatarajia kutoa ujumbe wake kuhusu mkakati wake wa kuwezesha wanawake kiuchumi katika Kongamano la Kizazi chenye Usawa wa Kijinsia linalotarajia kufanyika kuanzia Juni 30 hadi Julai 2, 2021,Paris nchini Ufaransa.
Akizungumza leo wakati wa kutangaza kongamano hilo la kihistoria Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Liberata Mulamula amesema ujumbe wa Tanzania kwenye kongamano hilo utaongozwa na Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango ambaye anamwakilisha Rais Samia.
Amesema kongamano hilo litajadili na kutoka na malengo ya nini kifanyike katika kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
“Wakuu wa nchi mbalimbali, taasisi ,mashirika,wanaharakati wa masula ya haki na jinsia watakutana katika Jiji la Paris nchini Ufaransa na kongamano hilo kinafanyika ikiwa imepita miaka 26 baada ya kufanyika Kongamano la Beijing nchini China.
“Kutakuwa na mijadala inayohusu usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali. Kwa Tanzania Rais wetu kwa niaba ya Serikali amechagua eneo la ambalo linahusisha kuongeza nguvu ya wanawake katika uchumi ,haki zao ,kuwa na usawa wa kushiriki katika uchumi, uchumi unaozingatia haki ili kupata maendeleo.
“Kuwawezesha kumiliki ardhi,kuwwezesha kumiliki ardhi , tunajua akina mama wengi wanajihusisha na biashara ndogondogo,hivyo baada ya mkutano huo utakwenda kujibu masuala ya kumuwezesha mwanamke na wakati tunakwenda kwenye hilo kongamano tayari Rais Samia alishaanza kuweka mikakati ya kuwawezesha wanawake,”amesema Waziri Mulamula.
Amesisitiza kutokana na ukubwa wa kongamano hilo, Rais alikuwa aende lakini kutokana na majukumu mengine ya kikazi, aliyonayo, amemtuma Dk.Mpango amuwakilishe na atakuwa na ujumbe ambao umesheheni usawa wa kijinsia, hivyo akiwa huko atawasilisha mipango ya Serikali ya awamu ya sita katika eneo hilo.
Alipoulizwa kuhusu ukatili wa kijinsia ukoje kwa Tanzania wakati wanaelekea kwenye kongamano hilo, Waziri Mulamula amejibu kwamba hana takwimu rasmi lakini ukatili bado upo huku akifafanua wakati wa janga la Corona lilipoanza shule zilifungwa na kuna taarifa ambazo zilisikika kuhusu kuongezaka kwa ukatili.
Amesema kuna mambo mengi yanayosababisha ukatili huo yakiwemo ya mila potofu ambazo zinachochea uwepo wa ukatili ambao unafanywa kwa wanawake ingawa na wanaume nao wanafanyia ukatili huo wa
Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania F’rederic Clavier amesema amefurahishwa na Serikali ya Tanzania kutangaza kushiriki kikamilifu kwenye kongamano hilo la kizazi cha usawa.
Balozi Clavier amesisitiza kongamano hilo la usawa wa kijinsia linakuja miaka 26 baada ya kongamano la Beijin ambalo pamoja na mafanikio yake bado kuna changamoto ya usawa,hivyo kongamano hilo limekuja wakati muhimu kwa kuhakikisha kunakuwa na malengo mengine kufikia usawa wa kijinsia.
“Lengo kuu la kongamano hilo ni kupata suluhu kutoka serikalini, taasisi,asasi ,wanaharakati watetezi wa wanawake kuhusu kizazi cha usawa.Nchi ya Ufaransa itafanya kazi kwa kushirikiana na nchi mbalimbali kufikia malengo hayo ikiwemo Tanzania,”amesema.
Aidha amesema katika kipindi cha miaka 26 tangu ulipofanyika mkutano wa Beijing kuhusu usawa kuna mafanikio ambayo yamepatikana lakini inahitajika nguvu zaidi kufikia kizazi chenye usawa, hivyo lazima kuwepo na mipango mingine kufikia usawa wa kijinsia.
“Na vijana ndio wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kwenye kuhakikisha kizazi chenye usawa kinakuwepo, hivyo mashirika yanayoongozwa na vijana wanatakiwa kuchachu ya kufikia usawa huo,”amesema Balozi Clavier.
Mwisho