Home LOCAL MAJALIWA: MIRADI 93 IMESAJILIWA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA

MAJALIWA: MIRADI 93 IMESAJILIWA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongea wakati wa Ufunguzi wa  Kongamano  la siku 100 za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambalo linatoa mrejesho kwa wadau wa Baraza la Wafanyabiashara (TNBC) lililofanyika kwenye kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Juni 27, 2021 Jijini Dar es Salaam

DAR ES SALAAM.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imesajili miradi 93 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.6 ambayo itaingiza ajira zaidi ya 24,600 kwa vijana.

Amesema kuwa hatua hiyo inatoa alama kwa wawekezaji wa nje kwamba kwa sasa urasimu katika sekta ya uwekezaji unaendelea kupunguzwa katika maeneo ya usajili wa makampuni pindi muwekezaji anapokusudia kuja kuwekeza nchini.

Waziri Mkuu ameyasema leo (Jumapili, Juni 27,2021) alipofungua Kongamano la siku 100 za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan lililofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Ametumia fursa hiyo kutaja miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha siku 100. 

Amesema mbali na miradi hiyo, pia Mheshimiwa Rais amefanya jitihada kubwa ya kuondoa tozo 232 zilizokuwa zinawakwaza wafanyabishara. “Tozo hizi zimeondolewa ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao hapa nchini.”

“Na haya yote ni katika kuongeza mzunguko wa fedha kwa Watanzania ambao wanashiriki katika shuhguli mbalimbali za kuimarisha uchumi wao.” 

Waziri Mkuu amesema katika kufanya kazi zake, Mheshimiwa Rais Samia ameendeleza mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi jirani ambapo ametembelea nchi za Kenya, Uganda na Msumbiji kwa lengo la kuimarisha urafiki na Mataifa ya jirani. Pia amepokea ujumbe kutoka nchi mbalimbali ikiwa ni alama ya mshikamano. 

Amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia ameendelea kupanga mipango ya ujenzi wa miradi mipya katika siku 100 za uongozi wake ikiwemo kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa reli ya kimataifa kipande cha kutoka Mwanza mpaka Isaka, ujenzi wa meli mpya nne na ukarabati wa meli kongwe moja.

“Meli hizi zimewekwa katika maeneo yote, ziwa Victoria tuna meli moja ambayo ina uwezo wa kubeba tani 3000 za mizigo itakayotoa huduma kati ya Tanzania, Kenya na Uganda, pia meli nyingine ya MV Umoja ambayo awali ilikuwa inakwenda Uganda nayo inakarabatiwa”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia ameanzisha mradi wa shule za sekondari za wasichana katika halmashauri zote nchini. Pia amesema Rais ametoa shilingi milioni 500 kwa kila jimbo kwa ajili ya kukarabati barabara ili kuboresha huduma za usafiri vijijini.

Akiongea katika Kongamano hilo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Eric Hamissi amesema kuwa katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia mamlaka hiyo imepokea barua za pongezi kutoka katika makampuni makubwa ya usafirishaji duniani ikiwemo ya Mediterrainian na Mesina Line kwa uboreshaji wa huduma bandarini hapo.

Amesema kuwa katika kipindi cha robo ya mwisho kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu wameweza kukusanya shilingi bilioni 236.8 sawa na ongezeko la asilimia 14 ukilinganisha na robo iliyopita ya kuanzia Januari hadi Machi ambayo walikusanya shilingi bilioni 203.

Naye, Kamishna wa Uhamiaji nchini Dkt. Anna Makakala amesema kuwa kwa kushirikiana na idara ya kazi wameanza kutoa vibali kwa kutumia mfumo wa kielektroniki ambapo katika kipindi cha kuanzia Mei 2021 hadi sasa wametoa vibali 3,377 vya kazi ukilinganisha na vibali 2166 vilivyotolewa katika kipindi kama hiki kwa mwaka jana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here