DODOMA.
Serikali imeombwa kupunguza kiwango cha matuta kilichopo katika barabara kutoka mkoa wa Songwe, Tunduma kwenda Sumbawanga Mjini kutokana na kuwa makubwa na mengi barabarani hali inayopelekea kuharibu afya za watumiaji wa vyombo vya moto katika barabara hizo.
“Barabara inayotoka mkoa wa Songwe-Tunduma kuelekea Sumbawanga mjini, tatizo la barabara ile ni matuta, yapo takribani 270 ukipita mara tatu tu kwenye ile barabara kiuno chako hakitakuwa na ushirikiano kabisa. Serikali itupunguzie yale matuta”
Akichangia katika hotuba ya bajeti, bungeni Jijini Dodoma, Mwakang’ata amasema hali ya matuta katika barabara nyingi nchini na kusababisha madereva na watumiaji wengine wa barabara kuharibu migongo na hata wamama wajawazito kuteseka wakati wa kwenda hospitalini.
Katika hatua nyingine, Mwakang’ata amasema serikali inapaswa kuboresha miundombinu iliyoko katika mkoa wa Rukwa kwa kutengeneza bandari, barabara za lami pamoja na Uwanja wa ndege wa Rukwa ili kurahisisha ufanyikaji wa biashara kati ya Rukwa na nchi jirani.
Aidha, Mwakang’ata ameipongeza serikali kwa kutenga bajeti yenye uhalisia kwa wananchi katika maeneo yote ya kiuchumi hususani kwa kupunguza faini za makosa ya waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda.
“Napenda kuwapongeza kwa suala la kuwakumbuka bodaboda, wamejiajiri wenyewe shida ilikuwa kuwakamata ovyo ovyo. Sasa tumeona wamepunguziwa faini isiishie hapo iendelee hata kwenye kuwakata kwa kosa moja mara moja sio mpaka ile elfu 30 izidi”
Pia ameitaka serikali iwapatie elimu waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda ili ziwasaidie katika kuendesha pikipiki hizo bila kusababisha ajali na pia kupunguza makosa mengi wanayoyafanya kutokana na kukosa elimu.
“Serikali pia iwaandalie mafunzo kwa ajili ya kuzijua sheria za barabarani, hawa wamekuwa wakijifunza tu siku tatu wanaingia barabarani bila kujua sheria za barabarani hivyo iwapatie elimu iwasaidie”
Mwakang’ata ameendelea kuipongeza serikali kwa kuwalipa madiwani kupitia serikali kuu huku akitumia nafasi hiyo kuiomba serikali iweze kuwaongezea posho kutokana na kazi nyingi wanazifanya madiwani nchini.
Kuhusu suala la walimu, Mhe. Bupe Mwakang’ata amesema serikali imefanya vizuri kuwapandisha walimu madaraja waliokuwa wanastahili kupandishwa madaraja kwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia walimu na watumishi wengine nchini kufanya kazi kwa bidii.