Home LOCAL WAKRISTO NA WATANZANIA WOTE WAASWA KUWAHESHIMU VIONGOZI WA DINI.

WAKRISTO NA WATANZANIA WOTE WAASWA KUWAHESHIMU VIONGOZI WA DINI.

 

Na: Maiko Luoga Mara.

Waumini wa Kanisa Anglikana na Watanzania wote nchini wametakiwa kuwaheshimu Viongozi wa Dini ambao wamekuwa wakiwaombea kwa mwenyezi Mungu kila wakati hasa Jamii na Taifa linapokutana na changamoto mbalimbali.

Wito huo umetolewa mei 23, 2021 na Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi alipokuwa Mgeni rasmi kwenye Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Canon Moses Yamo Masala kuwa Askofu wa pili wa Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Rorya iliyofanyika kwenye Kanisa Anglikana KOWAK Wilayani Rorya.

“Tuna jukumu la kuwaheshimu Viongozi wa Dini ambao wanakesha kila siku kutuombea na baadae watatoa hesabu zetu kwa mwenyezi Mungu, pia tunao wajibu wa kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ili tujenge Taifa la watu wema” alisema Profesa Palamagamba Kabudi.

Akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassimu Majaliwa, Waziri Kabudi alisema Serikali inampongeza Askofu Masala kwa kuchaguliwa kuwaongoza Waumini wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Rorya na kuahidi kumpa ushirikiano ili kutimiza wito wake alioitiwa na Mwenyezi Mungu. 

Canon Moses Yamo Masala Askofu wa pili wa Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Rorya katika kutekeleza majukumu yake ya kiroho, amewahakikishia kuwapa ushirikiano wa karibu Waumini wa Kanisa hilo na kusema ataendeleza mema yote yaliyoachwa na mtangulizi wake aliyekuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi hiyo Hayati John Adiema aliyefariki Dunia Tarere 12 Septemba 2020.

“Naomba kuwahakikishia Waumini wa Kanisa letu nitawapa ushirikiano wa kutosha ili tuweze kutimiza lengo tuliloitiwa na Mwenyezi Mungu la kutangaza injili yake, pia tutaendeleza kazi njema iliyofanywa na Hayati Baba Askofu John Adiema mtangulizi wetu” alieleza Askofu Moses Masala.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Dkt, Maimbo Mndolwa aliyeongoza Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu Masala wa Dayosisi ya Rorya amesema Kanisa litaendeleza ushirikiano na Serikali ili kuisaidia kutekeleza majukumu yake kwa faida ya Watanzania wote.

Ibada hiyo imehudhuriwa na Maaskofu wa Kanisa Anglikana Tanzania kutoka Dayosisi mbalimbali nchini, Waumini pamoja na Viongozi wengine wa Dini kutoka Mkoa wa Mara ambao walialikwa kushiriki na Viongozi wa Serikali wakiwemo baadhi ya Wakuu wa Wilaya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here