Home LOCAL SERIKALI YATAMBUA MCHANGO WA KANISA ANGLIKANA TANZANIA YAAHIDI USHIRIKIANO,

SERIKALI YATAMBUA MCHANGO WA KANISA ANGLIKANA TANZANIA YAAHIDI USHIRIKIANO,

 Na: Maiko Luoga, MWANZA.

Serikali imesema inatambua kazi kubwa inayofanywa na Viongozi wa Dini nchini ya kuhakikisha wanawajenga Watanzania kiroho na kimwili hasa kipindi hiki ambacho kuna Changamoto nyingi za maadili katika Jamii.

Hayo yamesemwa mei 16, 2021 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt, Philip Mpango alipokuwa mgeni rasmi kwenye Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu wa tano wa Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Victoria Nyanza Jijini Mwanza.

“Kwa niaba yangu binafsi na Serikali naomba nitambue kazi kubwa ambayo Kanisa Anglikana Tanzania kupitia Maaskofu, Makasisi na wahudumu wote mmekuwa mkifanya ya kuhakikisha mnawahudumia Watanzania kiroho na kimwili hasa kipindi hiki chenye Changamoto nyingi za maadili” alieleza Dkt, Philip Mpango Makamu wa Rais.

Aidha Mhe, Mpango alitumia nafasi hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumpongeza Askofu wa tano wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza Jijini Mwanza Zephania Ntuza kwa kuaminiwa na Wakristo wa Dayosisi hiyo, huku akisema Serikali itatoa ushirikiano kwake na Kanisa Anglikana kote nchini ili kuwahudumia Watanzania kiroho.

“Pamoja na changamoto nyingi mlizopitia Dayosisi hii ya Victoria Nyanza lakini sasa mmempata Baba wa kiroho, Baba Askofu nakupongeza sana kwa niaba ya Mhe, Rais Samia Suluhu Hassan tunatambua una kazi kubwa ya kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa na kuliombea Taifa letu”

Akitoa hotuba yake ya kwanza Mara baada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa tano wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza Kasisi Zephania Ntuza, licha ya kuwashukuru Waumini wa Kanisa hilo kwa kumwamini amesema atafanya kazi hiyo kwa hekima na maarifa ili kukuza zaidi huduma ya Injili ya Kristo.

Askofu Ntuza alimweleza Makamu wa Rais kuwa maeneo ya Kanisa Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza yanavamiwa na watu wasio waaminifu na kuyafanyia kazi huku akiomba Serikali kuingilia kati na Makamu wa Rais Mhe, Philip Mpango ameutaka Uongozi wa Kanisa kuwasilisha kwake taarifa ya maandishi Sambamba na kuahidi kumtuma Waziri wa Ardhi kulishughulikia Jambo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya Waumini Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Dkt, Maimbo Mndolwa alimpongeza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt, Philip Mpango kwa kuaminiwa na Rais kushika nafasi hiyo huku akisema Watumishi wa Mungu wataendelea kuliombea Taifa na Viongozi wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here