Home BUSINESS NEEC YAWAHIMIZA WAFANYABIASHARA GEITA KUKITUMIA KITUO CHA UWEZESHAJI KILICHOPO MKOANI HAPO.

NEEC YAWAHIMIZA WAFANYABIASHARA GEITA KUKITUMIA KITUO CHA UWEZESHAJI KILICHOPO MKOANI HAPO.

GEITA

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi limewataka Wananchi na Wafanyabiashara kukitumia kituo cha Uwezeshaji Geita ili kuweza kutambua na kutumia fursa zinazojitokeza Mkoani hapo.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Ndg. Julian Mutunzi wakati akizungumza Wajasiriamali na waandishi wa habari katika Kituo hicho kilichopo maeneo ya Bombambili Geita mjini.

“Kituo hiki kimeanzishwa kutokana na maagizo ya Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim M. Majaliwa aliyoyatoa mwaka 2019 katika kongamano la Mwaka la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Mkoani Dodoma kuwa vianzishwe vituo vya Uwezeshaji katika kila Mkoa. Vile vile ni mojawapo ya makubaliano ambayo yaliingiwa kati ya Baraza na Mgodi wa Dhahabu wa Geita wakati wa uanzishaji wa mradi wa kuwaendeleza Wajasiriamali Mkoani Geita.” Alieleza Mkurugenzi.

Alisema kuwa Baraza liliingia makubaliano na Mgodi wa Dhahabu wa Geita ili kuwaendeleza Wananchi wa waweze kufahamu njia sahihi wanazopaswa kupitia ili wawe kupata Zabuni katika Mgodi huo. Lakini Mpango Mkakati unaeleza wazi kuwa mafunzo yanayotolewa kwenye mradi haimaanishi kwamba Mfanyabiashara ni lazima afanye biashara na Mgodi wa Dhahabu wa Geita ila yatamsaidia kupata Zabuni hata sehemu nyingine.

Alisisitiza kuwa kituo kimewekwa rasmi kwa ajili ya Wafanyabiashara wa Geita na Watanzania wote watakaopenda kupata huduma pale. 

Kituo pia kitahusika moja kwa moja na utoaji wa taarifa za Zabuni zitolewazo na Mgodi kwa sababu kuna ubao wa matangazo kwa ajili ya kazi hiyo. Kituo hicho pia kitakua na Taasisi mbali mbali ambazo zinaweza kuwasaidia Wafanyabiashara kurasimisha Biashara zao ili kuziongezea thamani na hatimaye kuongeza Mtaji.

Aliongeza kuwa katika kuhakikisha Wananchi wanakifahamu kituo hicho cha Uwezeshaji Baraza linatumia njia mbali mbali kukitangaza kituo. Baraza kwa kushirikiana na Mgodi tumeshafanya matangazo kwa siku mbili mfululizo katika mitaa ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Halmashauri ya Mji wa Geita. Maeneo yaliyoyapitiwa ni kama Kasamwa, Mwatulole, Shilabela, Soko la Madini, Miti Mirefu, Nzela, Nyamkumbo na Katoro. Lakini bado kuna umuhimu wa kurudia ili kuweza kuwafikia Wananchi wengi zaidi. Sio hilo tuu lakini na vyombo vya habari vimekuwa vikishirikiana na sisi kuhabarisha watu kuhusu kituo hiki na shughuli zinazofanyika hapa tangu mwanzo wa mradi hadi kufikia sasa.

Vile vile katika kituo cha Uwezeshaji kuna vifaa vya kisasa ambavyo vimefadhiliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita ili kuwasaidia Wananchi katika upatikanaji wa taarifa lakini pia kuna maafisa wa Baraza na Taasisi nyingine kwa ajili ya utoaji wa Huduma.

Tangu mradi huu kuanza Wafanyabiashara zaidi ya 300 wameshapatiwa huduma kituoni hapa kuanzia namna ya kuanzisha biashara hadi kufikia urasimishaji. 

Nae mmoja wa wanufaika wa mradi na kituo cha Uwezeshaji Bibi. Rachel Nelly Andrew alisema kwa muda mrefu Wafanyabiashara wa Geita walikuwa hawajui taratibu za kurasimisha Biashara zao na umuhimu wake hivyo ujio wa mradi na kituo umeleta ukombozi mkubwa Mkoani hapo. Kwani kwa sasa wamejua hata umuhimu wa uanzishaji wa kongano (Clusters) ili kufikia malengo ya pamoja na kutimiza mahitaji ya mteja. Anaamini kuwa kwa mafunzo waliyoyapata yataenda kuwa na manufaa kwao na hatimaye kujiinua Kiuchumi.

Mkurugenzi aliushukuru Mgodi wa Dhahabu wa Geita kwa kufadhili mradi na vifaa vya kituo cha Uwezeshaji. Alifafanua kuwa Mgodi wa Dhahabu wa Geita uliopo chini ya Anglogold Ashanti unatekeleza sera ya Uwezeshaji ambayo ina kipengele cha uhusishwaji wa Wananchi katika miradi ya kimkakati lakini pia kuwawezesha Wananchi wa eneo husika kuinuka kiuchumi ambapo Mgodi umetoa fursa kwa Wafanyabiashara wa Geita kupata weledi, taarifa, elimu na mambo ya msingi katika Biashara na huu ni Uwezeshaji mkubwa mno.

Hadi tunavyotoa taarifa hii tumefikia hatua ya kuwakabidhi Wajasiriamali kwa Wafanyabiashara wenye uzoefu zaidi kwa ajili ya kuwalea na kuwapa ushauri unaostahili ili kukuza Biashara zao na yote haya tumeyafanya katika kituo cha Uwezeshaji kwa ufadhili wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here