Home LOCAL WAZAZI WAASWA KUWEKA MSUKUMO WA KUTOA ELIMU YA AFYA YA UZAZI KWA...

WAZAZI WAASWA KUWEKA MSUKUMO WA KUTOA ELIMU YA AFYA YA UZAZI KWA VIJANA   SHULENI KUEPUSHA MIMBA ZA UTOTONI

Na. Faustine Gimu,Elimu ya afya kwa Umma.

Wazazi  wameaswa kuweka msukumo wa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana  walioko shuleni ili kuwajengea afya imara na kuepusha mimba  za utotoni  na mimba zisizotarajiwa.

Wito huo umetolewa mkoani Morogoro na Afisa wa  mpango wa afya shuleni kutoka Wizara ya Afya,Magdalena Dinawi  katika kikao kilichoandaliwa na wizara ya afya  cha kujadili mpango   wa kusogeza mahusiano na mawasiliano ya afya ya uzazi baina ya mzazi na mtoto kilichokutanisha wadau mbalimbali  ikiwemo viongozi wa dini ,asasi za kiraia,taasisi zilizochini ya Wizara ya afya pamoja na wizara za kisekta ikiwemo Wizara ya Maendeleo ya Jamii,jinsia ,wanawake na makundi maalum pamoja na Wizara ya Elimu.

Dinawi amesema ni jukumu la kila mzazi kutoa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi kwa vijana balehe kwani pamekuwepo na changamoto ya kutopata taarifa muhimu kuhusu masuala ya afya ya uzazi kwa vijana .

“Ni jukumu letu kama wazazi na walezi kutoa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi  kwa vijana balehe kwani kuna changamoto nyingi ikiwemo kukosa taarifa kuhusu mabadiliko ya mwili na changamoto ya ongezeko la vichocheo ndani ya mwili hali ambayo inaweza kumpelekea kijana kujiingiza kwenye vitendo hatarishi vinavyoweza kumsababishia madhara ikiwemo mimba za utotoni pamoja na maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo UKIMWI”amesema.

Kwa upande wake mkufunzi wa kitaifa wa afya ya uzazi kwa vijana Dkt.Taramael Ndossi amesema katika ulimwengu wa sasa kuna changamoto ya vijana kukosa malezi ya wazazi kutokana na muda mwingi kuutumia shuleni hivyo mpango wa elimu ya afya ya uzazi  shuleni utasaidia kuelimisha wazazi na walimu namna nzuri ya kuwapatia elimu ya afya ya uzazi vijana walioko shuleni.

“Mtoto anakaa bweni anakulia bweni ,kwa hiyo huu mpango wa elimu wa afya shuleni  umekuja na wazo kuwa kumbe tunaweza tukaelimisha wazazi,tukaelimisha na walimu na kuwafundisha mbinu za mawasiliano ili waweze kuwasiliana na vijana wetu kuhusu afya ya uzazi”amesema.

Kwa upande wao baadhi ya wawakilishi kutoka wizara za kisekta akiwemo afisa maendeleo ya jamii mwandamizi  kutoka Wizara ya Maendeleo ya jamii ,jinsia,wanawake na makundi maalum Victor  Rugarabamu amesema mtu wa kwanza mwenye jukumu la malezi kwa mtoto ni mzazi  huku mwakilishi kutoka wizara ya Elimu Joel Mwamasangula  akisema   wazazi hawapaswi kujisahau suala la malezi wanapowapeleka watoto shule.

MWISHO

Previous articleAMEWATAKA WALIMU KUTOKOMEZA ZIRO ILALA 
Next articleTPDC YAENDESHA ZOEZI LA UTOAJI ELIMU YA MANUFAA, ULINZI NA USALAMA WA MIUNDOMBINU YA GESI ASILIA KWA VIJIJI VYA MKOA WA LINDI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here