Home BUSINESS WAKULIMA 590 IGUNGA WAJIUNGA MFUKO WA BIMA YA AFYA

WAKULIMA 590 IGUNGA WAJIUNGA MFUKO WA BIMA YA AFYA

Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Igembensabo Juma Mrisho (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Union hiyo Samwel Mirei (wa kwanza kulia) na Mhasibu Mkuu Fabian Kanijo (kushoto).
Na: Lucas Raphael,Igunga.

WAKULIMA 590 wa zao la Pamba wamejiunga na huduma ya Bima ya Afya iliyoboreshwa ili kupata huduma bora za matibabu kwa kipindi cha mwaka mzima na wategemezi wao wilayani Igunga Mkoani Tabora

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Pamba Igembensabo, George Kihimbi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliotembelea Ushirika huo jana.

Alisema kupitia mpango huo, vyama vya msingi 23 vya wakulima (AMCOS) ambavyo ni wanachama wa ushirika huo vyenye wanachama 590 na wategemezi 180 wamepata Bima ya Afya kwa ajili ya kupata matibabu kwa mwaka mzima.

Alibainisha mkakati wao katika msimu huu mpya wa kilimo kuwa ni kuendelea kuhamasisha wakulima wengi zaidi katika Wilaya za Nzega na Igunga kujiunga na Mfuko huo wa CHF ili kunufaika na huduma za afya.

Kihimbi alifafanua kuwa katika kuhakikisha wanachama wao wanapata huduma hizo bure kwa mwaka mzima waliingia mkataba na Mfuko huo na Benki ya Posta kwa ajili ya kuwapatia Bima wakulima wa zao hilo.

‘Bima ya afya ni muhimu sana kwa kuwa itasaidia wakulima kupata huduma za matibabu wakati wote pasipo kulipia gharama nyingine tena wanapougua, na wakiwa na afya njema wataongeza uzalishaji wa mazao yao’, alisema.

Aidha katika kuhakikisha Igembensabo inakuwa na mtaji wa kutosha ili kusaidia wakulima wa zao hilo katika wilaya za Nzega na Igunga, alisema wamewekeza kiasi cha sh mil 5 katika Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) na kununua hisa 1000 na wanatarajia kununua hisa zingine zaidi ya 400 za sh mil 2.

Awali akielezea mikakati yao Meneja Mkuu wa Chama hicho Juma Mrisho alisema wanakusudia kununua mashine kubwa ili kuanzisha mradi wa kukoboa mchele na kufungasha katika mifuko ya saizi tofauti na kuuza ndani na nje ya nchi.

Aidha alisema wanatarajia kuanzisha na kuendeleza kilimo cha zao la alizeti ambapo watalima shamba lenye ukubwa wa ekari 50 katika wilaya ya Nzega na ekari 100 za shamba la pamba katika wilaya ya Igunga.

Mrisho aliongeza kuwa wanampango wa kuanzisha shughuli za ukusanyaji wa pamba kwenye AMCOS na kuichambua, na hili linaenda sambamba na kurejesha Kiwanda cha Pamba cha Manonga Ginnery, juhudi za kukirejesha zinaendelea.

Mwisho.

Previous articleWANANCHI KIJIJI CHA NAMIJATI WILAYANI NANYUMBU WATOA YA MOYONI BAADA YA RAIS SAMIA KUWAPELEKEA MRADI WA MAJI, WASEMA ITAKUWA MARA YA KWANZA KUONA MAJI YA BOMBANI
Next articleRC KUNENGE AKEMEA UPANDISHAJI BEI ZA VYAKULA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here