Home LOCAL AHIMIZA VIWANJA VYA MICHEZO KUJENGWA-MHE.NDUMBARO

AHIMIZA VIWANJA VYA MICHEZO KUJENGWA-MHE.NDUMBARO

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI ipo katika mkakati wa kuhakikisha kila halmashauri inakua na kituo cha michezo kitakachojumuisha michezo yote na mkakati huo utakapokamilika utaletwa katika bajeti ya mwakani na utaanza kutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo sekta binafsi.

Mhe. Dkt Ndumbaro ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma leo Septemba 6, 2024 wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Mhe. Stella Simon Fiyao aliyetaka kujua lini Serikali itajenga uwanja wa michezo wilayani Ileje.

Mhe. Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa Serikali inaendelea na ukarabati wa viwanja vya Uhuru na Benjamin Mkapa pia ujenzi uwanja wa Arusha wa mpira wa miguu (Arusha Stadium) na kukarabati viwanja vingine vitano (5) vya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027.

Aidha, ameishauri Halmashauri na Wilaya ileje kutenga fungu katika bajeti yake ili kutekeleza mradi ya ujenzi wa uwanja wa michezo kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo akiongeza kuwa Wizara ipo tayari kuwapatia wataalam wa miundombinu ya michezo wa kuwashauri kabla na wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo.

Katika hatua nyingine amezipongeza Halmashauri za Wilaya ya Kinondoni (Uwanja wa KMC Stadium), Bukoba Mjini (Uwanja wa Kaitaba), Nyamagana (Uwanja wa Nyamagana), Halmashauri ya Mji-Babati (Tanzanite Stadium) na Namungo (Majaliwa Stadium) kwa kuonesha mfano bora na wa umiliki na uendeshaji wa viwanja vya michezo vya kisasa.

 

Previous articleNAIBU KATIBU MKUU CCM AANZA RASMI ZIARA SHINYANGA
Next articleRAIS DKT.SAMIA AZUNGUMZA NA WAWEKEZAJI WA MAKAMPUNI CHINA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here