Home BUSINESS SHIRIKA LA POSTA LAPONGEZWA KWA MASHIRIKIANO NA SEKTA BINAFSI

SHIRIKA LA POSTA LAPONGEZWA KWA MASHIRIKIANO NA SEKTA BINAFSI

Naibu Waziri wa Habari, Mawasilaino na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi ameshuhudia hafla ya utiaji saini wa mashirikiano kati ya Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Kampuni ya Azam Pesa tukio ambalo limefanyika katika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es salaam leo Julai, 17, 2024.

Na: Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Salaam

NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amelipongeza Shirika la Posta Tanzania (TPC) kwa kutekeleza falsafa ya 4R za Rais Samia hasa ile ya Mabadiliko (Reforms) kwa ubunifu wa kuboresha utendaji wa Shirika hilo kwa kuingia mashirikiano ya kibiashara na Sekta binafsi.

Mhandisi Mahundi amezungumza hayo wakati akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Nape Nnauye kuzindua na kushuhudia hafla ya utiaji saini mkataba wa kibiashara kati ya Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Azam Pesa iliyofanyika leo Julai 17, 2024.

Amesema kuwa ushirikiano baina ya TPC na Azam Pesa utaenda kuzinufaisha pande zote mbili za mashirikiano kwa kuongeza wigo wa wateja, kuongeza mapato na kuimarisha mzunguko wa kifedha kuanzia kwa mwananchi wa kawaida hadi mwenye kipato cha kati na cha juu kwa ajili ya urahisishaji wa shughuli za maendeleo ya mtu mmoja mmoja, na Taifa kwa ujumla.

“Nitumie nafasi hii kuipongeza kampuni ya Azam Pesa kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali kupitia Shirika la Posta Tanzania, na kwa niaba ya Serikali niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kuboresha Sera na Miongozo mbalimbali kwa maslahi ya Wananchi wote Watanzania”, amezungumza Naibu Waziri huyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema kazi ya Serikali kupitia Wizara hiyo ni kuipeleka nchi katika uchumi wa kidijiti na mashirikiano hayo ni moja ya njia ya kuipeleka nchi kwenye uchumi usiotumia fedha ngumu yaani “cashless economy”.

Aidha, Bwana Abdulla amemuelekeza Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania kutumia mashirikiano hayo kuongeza mzunguko wa matumizi ya fedha kidijitali kwa kuangalia namna ya kulihudumia eneo la wafanyabishara wa kariakoo na kuwajumuisha kwenye matumizi ya fedha kidijitali.

Naye Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bwana Maharage Chande amesema mashirikiano hayo na Azam Pesa ni sehemu ya mkakati wa Shirika kukuza mapato kutokana na biashara ya barua na vifurushi kupungua kutokana na mabadiliko ya teknolojia.

Mkurugenzi wa Azam Pesa, Bw. Ibrahim Malando amesema kupitia kampeni ya Ilipo Tupo, sehemu yeyote ilipo ofisi ya Shirika la Posta basi huduma ya Azam Pesa pia ipo, ambapo mawakala na wateja wataweza kujisajili na kupatiwa huduma za kifedha na malipo mbalimbali ya Serikali kupitia kauli mbiu ya “Huduma za Kifalme, kwa Bei za Kizawa”.

Previous articleKAMPUNI YA SHERIA YA KIGENI YADAIWA KUJINUFAISHA KUPITIA MADAI YA KUWATETEA WAHANGA WA UKIUKWAJI WA HAKI ZA KIBINADAMU MGODI WA NORTH MARA
Next articleKUELEKEA KILELE CHA KUPINGA BIDHAA BANDIA, WANANCHI WATAKIWA KUACHA KUZITUMIA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here