Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM
TUME ya Taifa ya Ushindani (FCC) wamesaini makubaliano ya ushirikiano na Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI), wa kiutendaji katika kuboresha mazingira ya uwekezaji wa viwanda na kudhibiti uzalishaji wa bidhaa bandia.
Makubaliano hayo yamefanyika katika hafla fupi kwenye Ofisi za FCC Leo Juni 5, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Akizumza na waandishi wa Habari muda mfupi kabla ya kusaini makubaliano hayo, kurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, amesema lengo la kusaini makubaliano hayo ni kuhakikisha kila mmoja anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi kukuza viwanda na kudhibiti bidhaa bandia.
“Kusainiwa wa makubaliano haya kutawezesha kufikia malengo ya serikali ya Rais Dk.Samia ya kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda.Mahusiano haya yatahusu namna bora ya kubadilishana taarifa hususan utekelezaji wa sheria mbili ambazo FCC tunazisimamia ikiwemo ya Ushindani na ya alama au nembo ya bidhaa zinazowahusu wenye viwanda,” amesema.
kuhusu Sheria ya bidhaa bandia, Erio amesema kuwa sheria hiyo inatumika kuzuia bidhaa hizo zinazoingia kupitia mipaka ya nchi na kutozalishwa nchini, na kusisitiza kuwa makubaliano hayo yatasaidia kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji wenye tija na kukuza ajira, fursa ya uchaguzi wa bidhaa na kukuza uchumi wa nchi kupitia viwanda.
“Tunahakikisha tunadhibiti vitu ambavyo vinaweza kuathiri wawekezaji ikiwemo ukiukaji wa sheria na makubaliano kuhakikisha havifanyiki”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye viwanda Nchini (CTI), Mhandisi Leodgar Tenga, ameipongeza FCC kwa kufanikisha kusainiwa kwa makubaliano hayo yanayotokana na ushirikiano mzuri wa Taasisi hizo mbili.
“kufanikiwa kwa makubaliano haya ni fursa kubwa ya kuhakikisha kuwa mazingira ya uwekezaji wa viwanda yanalindwa na kufikia azma ya Serikali katika sekta ya viwanda ili kuchochea ukuaji wa uchumi” amesema Tenga.