Home LOCAL WAZIRI UMMY AAGIZA MAGARI YA WAGONJWA YALIYOTOLEWA NA SERIKALI YAKATIWE BIMA YA...

WAZIRI UMMY AAGIZA MAGARI YA WAGONJWA YALIYOTOLEWA NA SERIKALI YAKATIWE BIMA YA AJALI

Na: Emmanuel Malegi – DODOMA

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameelekeza magari yote ya wagonjwa nchini yaliyotolewa na Serikali yanakatiwa Bima ya ajali ili iweze kusaidia katika matengenezo pale yanapopata ajali au kuharibika.

Waziri Ummy amesema hayo leo tarehe 16 Novemba, 2022 jijini Dodoma wakati akikabidhiwa magari 8 ikiwemo gari la wagonjwa yenye thamani ya Shilingi Milioni 500 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika ambayo yatatumika katika kujenga uwezo wa nchi wa kujiandaa,kugundua na kukabiliana na maafa na majanga ya afya ya jamii.

Waziri Ummy ameonekana kusikitishwa na taarifa za kuharibika kwa magari ya wagonjwa ambayo yametolewa na Serikali katika Halmashauri mbalimbali nchini ili yaweze kutoa huduma kwa wagonjwa wa maeneo husika lakini inakua tofauti na matarajio yaliyokusudiwa kwani mengi yanapata ajali au kuharibika na kuachwa bila matengenezo.

“Naumia sana kuona magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) tuliyonunua kwa bei kubwa yanakua hayakatiwi Bima na matokeo yake yakipata ajali au kuharibika yanatekelezwa. Kwahiyo nataka ‘Ambulance’ zote nchini zilizotolewa na Serikali zikatiwe Bima”. Amesisitiza Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuandaa mafunzo kwa madereva watakaoendesha magari hayo yaliyotolewa na WHO kuwa na mwitikio wa dharura katika majanga ya kiafya na ajali ili kuweza kukabiliana na maafa kwa haraka na kuweza kuokoa Maisha.

Pamoja na hayo Waziri Ummy amelishukuru Shirikia la Afya Duniani (WHO) kupitia kwa Kaimu Mwakilishi Mkazi wa WHO Tanzania Dkt. Zabulon Yoti kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa kutoa vifaa ikiwemo magari hayo ili kuweza kuimarisha hali ya utayari wa nchi katika kukabiliana na dharura na majanga ya afya ya jamii.

Mwisho, Waziri Ummy ameendelea kusisitiza ushiriki wa Sekta zote muhimu nchini katika kupambana na kukabiliana na majanga yanayoathiri afya ya jamii kwani hayahusu sekta ya afya peke yake.

Previous articleASILIMIA 70 YA MAGONJWA YA MILIPUKO YANATOKANA NA UCHAFU
Next articleWAZIRI MKUU AITAKA NHC KUSHIRIKISHA WABIA WENYE UWEZO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here