Home BUSINESS MRAJISI MKUU WA VYAMA VYA USHIRIKA DKT NDIEGE AKAGUA MAGHALA YA KUKUSANYA...

MRAJISI MKUU WA VYAMA VYA USHIRIKA DKT NDIEGE AKAGUA MAGHALA YA KUKUSANYA KOROSHO WILAYANI TUNDURU,ATAKA USAWA KWA WATUNZA MAGHALA WALIOTEULIWA ILI KUTENDA HAKI

 

Na: Muhidin Amri, Tunduru

MRAJISI Mkuu wa vyama vya Ushirika nchini Dkt Benson Ndiege amesema,watunza maghala watakaobainika kufanya udanganyifu katika msimu wa mauzo ya korosho  watachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufungiwa na kutojihusisha na shughuli za ukusanyaji wa zao hilo.

Dkt Ndiege,ametoa kauli hiyo jana mara baada ya kukagua maghala mbalimbali ya kukusanya na kuhifadhi korosho katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Dkt Ndiege,amelazimika kutoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko ya kutoka kwa baadhi ya wachukuzi wa ghala la Export linalotumiwa na kampuni ya Splendors Control Ltd kuwa ,shughuli za kupokea korosho zinafanyika taratibu ikilinganisha na maghala mengine.

Alisema, maghala yote yaliyoteuliwa yana haki  sawa ya kupokea mzigo wa korosho na kuwaasa viongozi wa vyama vya msingi kuacha upendeleo kwa watunza maghala kwani wote wana haki ya kupokea  korosho zinzotoka kwenye vyama vyao.

Amewataka viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika  na Chama Kikuu cha Ushirika wilayani humo(Tamcu), kusimamia na kuweka mazingira  mazuri ili zoezi hilo lifanyike kwa uwazi na usawa ili kuondoa malalamiko.

Awali mwakilishi wa wachukuzi  katika ghala  la Export Said Mohamed alisema, katika ghala hilo shughuli za kukusanya korosho zimesimama ikilinganisha na maeneo mengine, jambo linalowafanya kuishi maisha magumu za familia zao.

Naye meneja wa kampuni ya Splendors Control Ltd Grace Tarimo alisema, hadi sasa katika ghala hilo korosho zilizouzwa ni tani 1,193 na kilo 229 na ambazo hazijauzwa ni tani 9 na kilo 975.

Hata hivyo alieleza kuwa,changamoto kubwa wanayokutana nayo ni mapokezi ya mzigo kutokuwepo kwa usawa kwenye mgawanyo kwani  baadhi ya maghala yanapokea mzigo kidogo na katika ghala hilo wanakaa hata siku mbili bila kupokea mzigo.

Alisema,hawafahamu sababu  ya ghala hilo kazi ya kupokea  korosho kwenda taratibu kwa kuwa wenye jukumu  la kusimamia kazi hiyo ni Chama kikuu cha Ushirika wilayani humo (Tamcu).

Tarimo ameiomba serikali,kuangalia idadi ya maghala katika wilaya hiyo kulingana na uzalishaji na Chama kikuu kuweka usawa wa mzigo kwa kila ghala na kufahamu mzigo uliposhushwa kama ilivyoelekezwa na kufanya hivyo watapunguza tatizo hilo.

Kwa upande wake meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika(Tamcu)Iman Kalembo alisema, changamoto hiyo inatokana na baadhi ya vyama vya msingi  kuchagua msafirishaji wa korosho kwenda ghalani na watunza maghala kutumia ujanja ili wapate mzigo mkubwa.

Previous articleMABALOZI WANAWAKE WAAHIDI KUIUNGA MKONO TAASISI YA ZMBF
Next articleDKT. ASHIL AFUNGA RASMI MAADHIMISHO YA SIKU YA VIWANGO DUNIANI JIJINI DAR
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here