Tuzo ikikabidhiwa. Katikati ni Mlezi wa TAMUFO, Dk.Frank Richard ambaye ni Mume wa Stella.
Na: Dotto Mwaibale.
CHAMA cha Hati Miliki Tanzania ( COSOTA) kimemtunuku Tuzo ya Heshima Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuzi Tanzania (TAMUFO) Stellah Joel kutokana na mchango wake katika kuhamasisha maendeleo ya muziki nchini.
Akizungumza wakati akikabidhi Tuzo hiyo Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa COSOTA Filemoni Kilaka alisema wamemtuma Tuzo hiyo Stella Joel kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhamasisha maendeleo ya muziki.
“Stella Joel ambaye ni Mwanzilishi na Katibu Mkuu wa Taasisi ya TAMUFO amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha maendeleo ya muziki kwa kushirikiana na COSOTA na kuhakikisha Wanamuziki Wanasajiliwa na ili watambuliwe na Serikali ndio maana tukaona jitihada hizo zisiende bure tumtunuku tuzo hii” alisema Kilaka.
Alisema kazi anayoifanya Joel ni kubwa kwani anawiwa kuona kila mwaanamuzi ananufaika na kazi yake na kupata malipo kutokana na matumizi ya kazi hiyo na kila mwanamuziki analipa kiasi cha fedha ambayo itakusanywa na kuweza kuwanufaisha wenyewe.
Mwanamuziki Emmanuel Mbasha amewapongeza COSOTA kwa Kuutambua mchango wa Stella Joel na kuwa alistahili kupewa Tuzo hiyo kutokana na mchango wake katika Kuipambania Tasnia ya Wanamuziki.
“Dada huyu Stella ni wa mfano na tuna kila sababu ya kumuiga kwa haya anayoyafanya hakika ni kiongozi wa shoka” alisema Mbasha.
Dk. Frank Richard ambaye pia ni mume wake Stella ameishukuru COSOTA kwa Kuutambua mchango wa Stella na akaiomba Serikali na wadau wengine kuendelea kuwatia moyo viongozi wenye Taasisi zenye nia ya kusaidia kazi za Muziki.
Kwa upande wake Stella Joel amewashukuru COSOTA kwa Kumtunuku Tuzo ya Heshima ambayo ni ya Wanamuziki wote alioshirikiana nao kutekeleza majukumu yake kupitia TAMUFO na anatumia nafasi hiyo kuwaomba waendelee kudumisha upendo na ushirikiano ili kuipaisha tasinia hiyo.