NA: WAF- MOROGORO
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameweka wazi kuwa, agizo alilotoa Rais Samia kwa Wakuu wa Mikoa juu ya kusimamia suala la kuboresha lishe bora ni agizo la viongozi wote.
Dkt. Mollel amesema hayo leo kwenye Maadhimisho ya siku ya lishe ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Mikese Mkoani Morogoro na kuwataka Wadau kukutana na viongozi hao kuona namna gani ya kutekeleza agizo hilo.
“Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameshaelekeza Wakuu wa Mikoa namna ya kusimamia lishe kwenye Mikoa yao, agizo la Mhe. Rais hawajaagizwa Wakuu wa Mikoa peke yao, ni kwamba sisi Mawaziri, Manaibu Waziri na kila kiongozi asimame kwenye mstari wa mbele kutekeleza maelekezo ya Rais kwenye eneo la lishe.” Amesema Dkt. Mollel.
Ameendelea kusema kuwa, Wadau wa maendeleo wamekuwa wakifanya kazi nzuri katika suala la lishe ikiwemo kutengeneza mashine za kuchanganya virutubisho kwenye vyakula ili kutengeneza lishe bora, hivyo kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa na viongozi wengine kukaa pamoja kuona namna gani ya kuzitumia mashine hizo.
Ameendelea kusisitiza kuwa, mashine hizo za kuchanganya virutubisho licha ya kuboresha suala la lishe kwa wananchi hususan watoto litasaidia kuongeza ajira kwa vijana na Wanawake kwa kukuza kipato chao.
Sambamba na hilo Dkt. Mollel ametoa wito kwa wazazi kuwapa watoto lishe bora ili kuwajenga kimwili na kutengeneza Taifa lenye watu wenye akili, huku akisisitiza kuwa Dunia ya watu walioendelea ni kwasababu namba kubwa ya wananchi wao wana akili inayotokana na lishe bora.
“Kila Mkuu wa Mkoa anatamani kuona shule zake zinaongoza kwa elimu, kusimamia Walimu kuingia darasani tu haitoshi kuwa sababu ya kuongoza kielimu kama hatutasimamia suala la lishe bora kwa watoto wetu.” Amesema Dkt Mollel
Pia, ametoa wito kwa Wadau kuendelea kushirikiana na Serikali kwa karibu ili kusaidia kufikisha virutubisho vitavyowekwa kwenye vyakula kama uji wa watoto ili wapate lishe bora utaowasaidia kukuza kiwango cha uelewa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatuma Mwasa amekiri wazi kuwa licha ya Mkoa wa wake kuwa moja ya Mikoa inayofanya vizuri katika uzalishaji wa vyakula nchini bado kuna changamoto ya lishe duni inayotokana na ukosefu wa elimu juu ya lishe bora kwa wananchi hususan watoto.
Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kupeleka kiasi cha shilingi Bilioni 22 kwaajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi huku Bilioni 3 zikienda kwenye kuboresha huduma katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa, ambapo zimetumika kuboresha jengo la mapokezi wa wagonjwa wa nje, ujenzi wa ICU ya kisasa na jengo la kisasa la mama na mtoto.
Mwisho.