Mkurugenzi wa taasisi ya Usalama Barabarani (TARIS) Maliki Barongo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 21, 2022 kushoto ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kinondoni, Notker Kilewa.
Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kinondoni, Notker Kilewa katikati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 21, 2022 kushoto ni Mkurugenzi wa taasisi ya Usalama Barabarani (TARIS) Maliki Barongo na kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji ya Tosh, Mohamed Nassoro
Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji ya Tosh, Mohamed Nassoro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 21, 2022 kulia ni Mkurugenzi wa Kasi Media, Mohamed Ally
Mwanafunzi wa Shule ya Semianari ya Kiislamu ya Mtambani, Abul Robart Macha akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 21, 2022 jinsi atakavyoshirikiana na wenzia katika kueleimisha juu ya usalama barabarani.
Picha ya Pamoja.
WADAU na watumiaji wa barabara endapo watatimiza wajibu wao watasaidia taasisi ya Usalama Barabarani (TARIS) Kuweza kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 kwa kuhakikisha wanafuata sheria za barabarani.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na TARIS watatoa elimu mashuleni kwa sababu wanaamini wanapowafundisha wanafunzi, watakuwa mabalozi kwa wazazi wao na watu wengine wanaowazunguka hivyo wataongeza uwajibikaji katika kutekeleza sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 21, 2022 Mkurugenzi wa TARIS, Maliki Barongo amesema kazi inayofanywa na taasisi hiyo ni kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi yote ikiwemo madereva wa magari, bodaboda, wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Amesema Septemba 23, mwaka huu itafanya uzinduzi wa kampeni ya kutoa elimu katika shule mbalimbali za Msingi na Sekondari nchini, madereva wa magari, bajaji na bodaboda kwa lengo la kuyafikia makundi yote yanayotumia barabara.
Barongo amesema uzinduzi wa kampeni hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Novemba 2021, huko mkoani Arusha akiwataka wadau kushirikiana na jeshi la Polisi kutoa elimu ya usalama barabarani hivyo waliona wawe wa kwanza kutekeleza agizo hilo.
”Baada ya ufunguzi huu tutapita katika shule mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu lengo kupunguza ajali za barabarani kwani hivi karibuni kumekuwa na ajali nyingi zinazohusisha wanafunzi na makundi mengine.”
Amesema ajali hizo zimekuwa zikipoteza kwa nguvu kazi ya taifa na gharama kubwa za kurekebisha miundombinu na majeruhi wanaopelekwa hospitali.
Amesisitiza kuwa TARIS inawajibu wa kushirikiana na serikali ili kufikisha elimu hiyo kwani asilimia kubwa ya ajali za barabarani husababishwa na makosa ya kibinadamu hivyo wanapaswa kuwakumbusha watumiaji wa barabara wajibu wao katika kupunguza ajali.
Pia amesema madereva kupitia mafunzo kwenye vyuo pekee hayatoshi badala yake wanapaswa kupata elimu ya mara kwa mara ili kufuata sheria za usalama barabarani.
Kwa upande wake, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kinondoni, Notker Kilewa amesema Jeshi la Polisi lina jukumu kubwa la kulinda usalama wa raia na mali zao hata wakati zinapotokea ajali.
Amesema kuwa ajali zimeendelea kuwa tishio nchini hivyo kusababisha madhara makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
“Tunajukumu la kutoa elimu kwa makundi yote yanayotumia barabara kama vile madereva, watembea kwa miguu, abiria, wasukuma mikokoteni na wanafunzi ili kubadili tabia zao na kutii sheria zilizowekwa. Ajali zimeendelea kutokea kwa sababu ya mapungufu.” amesema Kilewa
Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji ya Tosh, Mohamed Nassoro amesema wataendelea kushirikiana na jeshi la polisi katika kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanafuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali.
Amesema ajali zinaacha wajane, yatima na kuleta hasara kwa taifa na jamii kwa ujumla hivyo watahakikisha elimu wanayoitoa inawafikia watu wengi jambo litakalosaidia nchi kuwa salama.