Na: Farida Mangube Morogoro.
Jeshi la polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia vijana wawili kwa tuhuma za kugushi vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya darasa la saba katika zoezi la usahili wa vijana wanaotakiwa kujiunga na jeshi la la kujenga Taifa JKT
Vijana hao wamekamatwa tarehe 5 mwezi wa 9 mwaka huu majira ya saa tano asubhi wakati wa zoezi la usahili wa vijana wanaotakiwa kujiunga na jeshi la la kujenga Taifa JKT ulifanyika katika viwanja vya Bwalo la Umwema JKT Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Fortunatus Musilimu aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Donald Charles Mayunga mwenyeji wa Lukobe Manispaa ya Morogoro na Hashim Hemed Mkande mkazi wa Jjijini Dar es Salaam wote wakiwa na umri wa miaka 18.
Alisema baada ya mahojiano ya muda mrefu na watuhumiwa hao walimtaja mmiliki wa steshenari anayefahamika kwa jina la Merry Banzi mkazi wa Kilakala Manispaa ya Morogoro mwenye umri wa miaka 54 kuwa ndiye aliyetengeneza vyeti hivyo.
“Baada ya kupata hizo taarifa jeshi la polisi lilikwenda mpaka kwa mfanyabiashra huyo na kumuhoji ambapo alikili kuhusika na utengenezaji wa vyeti hivyo bandia, ambapo baada ya kukili tulifanya upekuzi na kumkuta na vyeti bandia vya kuzaliwa vipatavyo 16 vyenye majina ya watu mbalimbali, vyeti 4 vya darasa la saba, vyeti 13 vya kumaliza kidato cha nne pamoja na mihuli 10 bandia ya taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo ya Musajili wa vizazi na vifo RITA.” Alisema kamanda Musilim.
Kamanda Musilim alisema bado jeshi la polisi linaendelea na upelelezi ili kuwakamata na kuwachukulia hatua wote wanaojihusisha za kugushi nyaraka za serikali kwa lengo la udanganyifu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Morogoro, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Wakili Msomi Albert Msando amewataka vijana wanaotafuta ajira kuacha tabia ya kugushi vyeti kwa lengo la kupata ajira kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha ameliagiza jeshi la polisi Wilaya ya Morogoro kufanya uchunguzi yakinifu ili kubaini mnyororo wa watu wote wanaofanya biashara hiyo haramu ya kugushi nyaraka za serikali kwa lengo la kujinufaisha.
“Nimelielekeza jeshi la polisi kuhakikisha kwamba wanapeleleza mpaka mtu wa mwisho anayefaidika na kugushi nyaraka tumekuwa na changamoto kubwa ya watu kugushi nyaraka, watu wanagushi mpaka mirathi, hati za nyumba sasa tunataka twende tukauondoe huu mtandao.” Alisema DC Msando
Dc Msando amezitaka taasisi za serikali pamoja na mashirika binafsi ambazo zinatilia shaka uhalali wa vyeti vya watumishi aua wanaofika kuomba kazi katika taasisi hizo kufika katika ofisi za mkuu wa wilaya ili kujilidhisha na uhalali wa nyaraka hizo.