Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kushoto,akikabidhi hati ya ardhi kwa Mkuu wa chuo cha Uhasibu Arusha Dkt Mwaitete Cairo kulia kwa ajili ya kuanza ujenzi wa chuo cha Uhasibu Tawi la Songea mkoani humo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Micheal Mbano kulia,akimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dkt Frederick Sagamiko baada ya kukamilisha kazi ya upimaji wa ardhi katika kitongoji cha Pambazuko kata ya Tanga eneo linalotarajia kujengwa kwa chuo cha Uhasibu Arusha-Tawi la Songea mkoani Ruvuma.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wa tatu kulia,Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho wa tatu kushoto,Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema wa pili kushoto na Mwenyekiti wa Baraza la chuo cha Uhasibu Arusha CPA Joseph Mwigune wa pili kulia wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Mkuu wa mkoa kukabidhi hati ya ardhi yenye ukubwa wa ekari 67 kwa Uongozi wa chuo cha Uhasibu Arusha kwa ajili ya kujenga chuo kipya cha Uhasibu Arusha Tawi la Songea,wa kwanza kulia Mkuu wa chuo hicho Dkt Mwaitete Cairo,kushoto Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michela Mbano.
Na: Muhidin Amri,, Songea
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,amekabidhi hati ya ardhi yenye ukubwa wa ekari 67 katika kitongoji cha Pambazuko kata ya Tanga Manispaa ya Songea kwa Uongozi wa chuo cha Uhasibu Arusha kwa ajili ya kujenga chuo cha Uhasibu mkoani humo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi hati hiyo kwa Mkuu wa chuo hicho Dkt Mwaitete Cairo,Brigedia Jenerali Ibuge amempongeza Rais Samia Hassan, kwa uongozi wake ambao umeanza kuonyesha dira kubwa katika mkoa huo na nchi kwa ujumla,kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
Mkuu wa mkoa,ameishukuru wizara ya elimu kwa kuona umuhimu wa kujenga chuo hicho kikubwa katika mkoa huo ambacho mara kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 4000.
Alisema,mkoa wa Ruvuma ndiyo unaoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara,kwa hiyo kuanzishwa kwake ni faida kubwa kwa kuwa wanafunzi na watumishi wa chuo watahitaji huduma mbalimbali ikiwamo chakula.
Ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuanza mchakato wa ujenzi wa haraka na kuhaidi kuwa,serikali ya mkoa itahakikisha inatoa ushirikiano mkubwa na wa karibu ili kazi ya ujenzi ianze na kukamilika haraka.
Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa,tayari serikali imeshapeleka huduma ya umeme na maji yanayotosheleza mahitaji wakati wa ujenzi na hata baada ya chuo hicho kukamilika kwani Serikali ya mkoa ina matumaini makubwa na uwekezaji unaokwenda kufanyika.
Ibuge,ametoa wito kwa wanachi wa mkoa huo kujiandaa kukitumia chuo hicho kupata elimu na huduma nyingine, badala ya fursa hiyo kuwanufaisha watu kutoka nje ya mkoa wa Ruvuma.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michela Mbano, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kuendelea kuwekeza miradi mbalimbali katika mkoa wa Ruvuma inayolenga kuchochea na kuharakisha maendeleo na kukua kwa uchumi wa mkoa huo.
Alisema,Manispaa ya Songea itawapa ushirikiano mkubwa wawekezaji wote watakao onyesha nia ya kutaka kuwekeza miradi na kufanya biashara katika manispaa hiyo.
Mkuu wa chuo hicho Dkt Mwaitete Cairo,amewapongeza viongozi wa Serikali ya mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na Manispaa ya Songea kwa kutoa ardhi hiyo bure kwa ajili ya kujenga chuo hicho.
“nawapongeza sana viongozo wa serikali ya mkoa wa Ruvuma kwa kutoa ardhi bure ili kujenga chuo cha Uhasibu,lengo letu tunatarajia kuanza kupokea wanafunzi ifikapo mwezi Agosti 2023,kwa kweli tunaipongeza sana serikali kwani hatujawahi kupata ardhi bure tangu tuanze mpango wa ujenzi wa vyuo vyetu”alisema Dkt Mwaitete.
Makamu Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho CPA Joseph Mwigune alisema,mpango uliopo ni kuhakikisha chuo hicho kinajengwa haraka ili kutoa nafasi kwa vijana mbalimbali wa mkoa wa Ruvuma na mikoa ya jirani kujiunga na chuo hicho mara kitakapokamilika mwa ujao.
Alisema, chuo hicho kitatoa huduma ya daraja la kwanza kama ilivyo kwenye vyuo vingine vya vya Babati na Dar es slaam ambapo ameishukuru Serikali ya mkoa wa Ruvuma kwa kutoa eneo hilo kwa ajili ya kujenga chuo.
Alisema, hayo ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan anayetaka huduma ya elimu inayotolewa na chuo hicho inawafikia wananchi kwa ukaribu zaidi kwa kuwa kutoka Ruvuma hadi Arusha au Dar es slaam ni mbali jambo linalosababisha baadhi ya watu kukosa fursa hiyo ya masomo.
MWISHO